NA ASIA MWALIM

Mabadiliko ya teknologia yameifanya serikali kubadili mitaala ya masomo mara kwa mara, ili ufundishaji uweze kuleta ufaulu mzuri wa masomo ya sayansi.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mjini Magharibi ‘B’ Mohamed Abdallah Mohamed, aliyasema hayo alipokua akizungumza na muandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar, ambapo alisema mabadiliko hayo yanakwenda sambamba na muktadha wa ukuaji wa elimu katika nyanja za kisayansi na kijamii.

Aidha alisema kufanya hivyo ni kuiboresha sekta ya elimu ili iweze kwenda sambamba na mahitaji ya wanafunzi kwa kuongeza uwezo wa teknelogia nchini pamoja na ufaulu wa masomo yao.

Alifahamisha kuwa Wizara ya Elimu katika kuhakikisha wanaenda sambamba na ukuaji wa sayansi na teknelogia, mitaala hiyo imeingiza  baadhi ya mambo muhimu na mengine kutolewa, ili kuendana na  wakati.

Alieleza kuwa Wizara ya Elimu ipo makini ili  kuhakikisha inaboresha sekta ya elimu ngazi zote nchini kutokana na kutanuka kwa sekta hiyo na ukuaji wa teknelogia.

Akizungumzia kuhusu kutumika kwa silabasi hizo alisema wadau  wa elimu wanapatiwa habari  zinazotolewa na wizara katika mambo yanayohusu elimu, hivyo wanapaswa kufuata utaratibu uliotolewa na wizara hiyo katika ufundishaji.

Aidha alisema wanafunzi wanapaswa kusoma kwa bidii na kuacha tabia ya kuchagua masomo, ili kuwajenga uwezo wa ufaulu vizuri mitihani yao kwa kupata taaluma zinazoendana na kasi ya mabadiliko ya kisayansi.

Mapema alieleza sababu za ufaulu mdogo kwa wanafunzi alisema ni kutokana na utoro, unaofanywa na baadhi ya wanafunzi, hivyo kukosa kuhudhuria masomo yao ipasvyo.

“Wapo wanafunzi wanatoka majumbani kwao  kuelekea skuli lakini wanaishia njiani na  wengine wanashindwa kuhudhuria vipindi vyote vya masomo ya kila siku” alisema.

Sambamba na hayo aliwataka wanafunzi kuendana na wakati ili kuyafikia mahitaji yao ya kupata elimu sahihi ili waweze kufika malengo husika.

Baadhi ya wanafunzi walisema masomo wanayosomeshwa siyo yanayotoka kwenye mitihani, hivyo inawapa mzigo mkubwa kwani idadi ya masomo yao ni kubwa.

Fatma Muhuidini kutoa skuli ya Maungani alisema kubadilishwa kwa mitaala kunawapa ugumu wa masomo mapya kipindi cha mitihani hali inayopelekea kufanya vibaya na kupata kiwango kidogo cha  maksi kwenye baadhi ya masomo.

“Unafika kwenye mitihani unakutana na mada hujawahi hata kuiona darasani kwa kweli hili linatukatisha tamaa ” alisema.