NA VICTORIA GODFREY

UONGOZI wa Chama cha Ngumi za Ridhaa mkoa wa Dar es Salaam (DABA) umesema mashindano ya majaribio yamepangwa kufanyika April 7 mwaka huu kwenye ukumbi wa CCM Amana Ilala ,Dar es Salaam.

Awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika Machi 20 mwaka huu na yalisogezwa mbele ili kupisha maombolezi ya siku 21 ya Hayati Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu.

Mwenyekiti wa DABA, Akalory Godfrey, alisema mashindano hayo yatashirikisha klabu mbalimbali kwa lengo la kuwaandaa na kuwaweka tayari mabondia kushiriki mashindano ya wazi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema mashindano hayo yatawapa nafasi makocha kuangalia kasoro za mabondia wao na kuzifanyia kazi ili kuleta ushindani mkubwa na kupata ubingwa.

“Kabla ya kuelekea kwenye mashindano ya mkoa, tutaanza mashindano ya majaribio ambayo yatakuwa ni kipimo cha makocha wa klabu kuimarisha wachezaji wawe na ushindani,” alisema Godfrey.

Alitoa wito kwa timu na klabu kutoa fursa kwa mabondia kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo.