NA MARYAM HASSAN

WAKURUGENZI watano wa kampuni ya Master Life Microfinance Limited, wanaotuhumiwa kwa makosa manne wanaendelea kusota rumande, ambapo ombi la dhamana yao litafikiriwa Aprili 22 mwaka huu kesi yao itakaposikilizwa tena.

Hayo yameelezwa na Jaji Aziza Iddi Suwed, mara baada ya washitakiwa hao kusomewa makosa yanayowakabili, ambapo jaji huyo alieleza kuwa ombi la dhamana litatolewa endapo upande wa mashitaka wa serikali utaridhia, kwa kuwasilisha hoja zao.

Wakurugenzi hao kwa mara ya kwanza walipandishwa mahakama ya mkoa Vuga mbele ya Hakimu Yesaya Kayange Aprili 8 mwaka huu ambapo waliposomewa makosa yao hawakutakiwa kujibu chochote.

Wakurugenzi hao ni Mzee Said Hassan (29), Joseph Alban Mwale (32), Abudu Abdalla Haji (31), Muslim Jaffar Abdul-rasul (54) na Kassim Abdi Kassim (33).

Mapema wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Mohammed Saleh kwa kushirikiana na Omar Makungu na Mohammed Haji waliwasomea washitakiwa hao makosa yao.

Upande wa mashitaka ulisisitiza kuwa bado upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.

Aidha umeeleza kuwa katika kikao kijacho watafanya marekebisho ya hati ya mashitaka katika kosa la nne ambapo wataunganisha na kifungu cha sheria ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi chini ya kifungu cha sheria namba 49 sheria nambari 7(1)(a) na 8(a).

Kwa upande wa wakili wa kujitegemea kwa washitakiwa hao Hassan Kijogoo aliiomba mahakama kuwapa dhamana wateja wake kwa sababu makosa waliyoshitakiwa si miongoni mwa makosa ambayo hawapaswi kupewa dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 151 (1) sheria nambari 7 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Alisema kwa sheria hiyo makosa yao hayakutajwa kwamba mtuhumiwa hapaswi kupewa dhamana.

Alisema ingawa kumefanyika marekebisho ya sheria nambari 1 ya mwaka 2021 ambayo yanahusisha makosa kama hayo, lakini wateja wake walitenda makosa hayo mwaka jana kabla ya marekebisho kufanyika.

Kijogoo alisimamia hoja zake kuwa sheria ya mwaka 2021 haiwezi kumuwajibisha mtu aliyetenda kosa tokea mwaka jana, hivyo aliiomba mahakama itumie vifungu vya sheria ili wapewe dhamana.

Kwa upande wake Said Mayugwa ambae nae anawasimamia washitakiwa hao alisisitiza juu ya kupewa dhamana washitakiwa hao kwa sababu wapo baadhi yao wagonjwa.

Alisema alitumia fursa hiyo kwa kuiomba mahakama kumpa ruhusa ya matibabu mshitakiwa Muslim Jaffar Abdul-rasul, kwa sababu hali yake si nzuri.

Baada ya kueleza hayo Jaji Aziza aliahirisha shauri hilo hadi Aprili 22 mwaka huu na washitakiwa wamerudishwa rumande.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani kwa makosa manne ikiwemo kukwepa kodi, kughushi nyaraka, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutakatisha fedha.

Itakumbukwa kuwa Machi 4 mwaka huu serikali ilichukua hatua ya kuizuia kampuni hiyo, kuendelea na shughuli zilizokuwa zikiendeshwa katika maeneo mbali mbali ya nchi kinyume na taratibu za nchi zilizowekwa.