Yabainika mishahara, wafanyakazi hewa
NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa makamanda watatu wa Idara Maalum za SMZ, baada ya kamati ya uchunguzi kubaini madudu kadhaa.
Waliotenguliwa ni :-
Kamanda wa Chuo cha Mafunzo, Ali Abdallah Ali, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU)

Kanali Ali Mtumweni Hamad

Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) Comodore Hassan Mussa Mzee

Akitoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, Dk.Mwinyi alisema aliunda kamati kufuatia taarifa za uwepo wa wafanyakazi hewa katika Idara Maalum za SMZ ili uhakiki wa idadi ya wafanyakazi na viwango vya mishahara inayotolea.
Alisema kuwa ripoti ya kamati imebaini wafanyakazi 381 waliokuwa wakilipwa mishahara bila ya kuwa katika utaratibu unaotakiwa kwa maana ya watumishi hewa.
Dk. Mwinyi alisema kwamba imebainika kuwa fedha zilizotumika kwa upotevu ni kiasi cha shilingi bilioni 2,235,725,000 kutokana na fedha zilizokuwa zikitumika kwa wafanyakazi hewa.
Alisema kwamba waliwahi kukamatwa baadhi ya maafisa katika nyumba ya mtu binafsi wakiwa wamewavisha sare za jeshi vijana na kuwapiga picha ili kuthibitisha kwamba ni waajiriwa.
Aidha alisema kamati ilikwenda kuhakiki ulipaji wa posho katika vikosi hivyo ambapo ilibaini wastani wa upotevu wa fedha kwa ajili ya posho kwa mwezi wa Disemba ni 304,135,939.
Alisema ilibaini kwamba kuna watumishi waliostaafu 12 bado walikuwa wakiendelea kupokea mishahara jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Alieleza kwamba hali hiyo imesababishwa na wahasibu wakuu wa Idara Maalum za SMZ kwa uzembe ama kwa kukusudia ambapo kwa misingi hiyo serikali imeingia hasara ya shilingi 44,610,280.00.
Dk. Mwinyi alisema kwamba mtumishi anapofukuzwa kazi hutakiwa kuwekewa kizuizi cha mishahara mara tu anapofukuzwa, lakini kamati imegundua kwamba wahasibu wakuu wa vikosi pamoja na waingizaji wa taarifa za mishahara huchelewesha mchakato huo kwa makusudi ili fedha hizo zitumike katika matumizi yao binafsi.
Alifahamisha kuwa wahasibu huwatengenezea madeni watumishi waliofukuzwa kazi na fedha hizo hukatwa na kupelekwa kwenye duka la kikosi na hatimae huingia mifukoni mwa wahasibu hao ambapo jumla ya fedha zilizopotea kwa aina hiyo ni kiasi cha shilingi 117,724,000.
Aidha, alisema kuwa Kamati imebaini kwamba kuna ukataji wa posho ya chakula kwa askari kapera kinyume na utaratibu kwani askari anapoajiriwa hukaa kambini kwa kipindi cha miaka miwili na kukatwa posho shilingi 70,000 kwa kila askari kwa kila mwezi fedha ambazo ni kwa ajili ya kujikimu.
Alisema kwamba kwa upande wa JKU Kamati imebaini kwamba jumla ya askari 771 walikatwa fedha za posho ya chakula bila ya kukaa kambini na fedha zao kiasi cha shilingi 539,700,000 kuingia mifukoni mwa watu wachache.
Pia, kamati hiyo imebaini kwamba maofisa na askari wananyimwa fursa ya kupata vielelezo vya taarifa za mishahara yao ikiwemo ‘pay slip’ hiyo imepelekea kwa baadhi ya askari hao kukatwa mishahara yao kinyume na utaratibu na kutokujua malengo ya makato hayo.
Dk. Mwinyi alisema kamati imefanyakazi vizuri na kugundua udhaifu sehemu nyingi na kwamba inatosha kwa yaliyobainika na kuagiza kuchukuliwa hatua za kisheria ambapo aliagiza wahasibu na waingizaji wa data wachukuliwe hatua za kisheria.