Wasema wako tayari sasa kugombea
HABIBA ZARALI, PEMBA
“KATIKA kuhakikisha wanawake wanapata nafasi za uongozi na kufikia asilimia 50 kwa 50, lazima jamii iwe na mwamko wa uthubutu kugombea nafasi mbalimbali na sio kusubiri kuteuliwa”, ni kauli ya baadhi ya wanawake niliozungumza nao katika makala haya.
Ni wakati sasa wa dunia kutambua umuhimu wa wanawake katika uongozi na kuendeleza uwezeshaji zaidi wa wanawake kuweza kuingia katika vyombo vya maamuzi.
Uzoefu unaonesha kuwa, wanawake wanapokuwa katika uongozi ni chachu ya kuondosha ubaguzi wa kijinsia na kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Si jambo la mzaha kuwa wanawake wanapowakilisha vizuri katika vyombo mbalimbali vya maamuzi kama vile mahakama, mabaraza ya vyombo vya kutunga sheria wanakuwa na mtazamo mpana na mawazo yenye kuhusisha kila nyanja,
Wanawake wenyewe wanasema kwa miaka mingi huogopa kujiingiza katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuishia kuwa wapiga kura tu kwa wanaume jambo ambalo kwa sasa linahitaji kutupiliwa mbali.
Wanasema licha ya mfumo dume kutawala katika jamii na vyama vya siasa ya kumuona mwanamke kama ni kiumbe asiye na uwezo wa kuwa kiongozi na wenye mamlaka hayo ni wanaume pekee umepitwa na wakati.
Kwa maana hiyo basi wanawake wenyewe wanahitajika kuwa na hamasa ya kufikia katika nafasi za kugombea kama vile katika majimbo na maeneo mengine ifikapo uchaguzi wa 2025.
Masuala mbali mbali yamekuwa yakiulizwa na wanaharakati wa kutetea haki za wanawake katika kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Haswa pale mikataba ya kimataifa na kikanda pamoja na sheria na katiba za nchi mbalimbali zimebainisha haki za wanawake za kushiriki katika kuwania nafasi za uchaguzi.
Baadhi ya mikataba hiyo ni pamoja na tamko la kimataifa kuhusu haki za binadamu ambalo limetamka kuwa binadamu wote wanahaki sawa za kisiasa bila ya kubaguliwa kwa njia yoyote ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa kijinsia.
Kwa mfano baraza la Umoja wa Mataifa lilisisitiza haki za wanawake za kisiasa katika mkataba wake wa haki za wanawake za kisiasa uliopitishwa mwaka 1952.
Umoja wa Afrika (AU), kwenye Mkutano Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika ‘SADC’ la jinsia na maendeleo la mwaka 2008, pamoja na mkataba wa nyongeza wa haki za wanawake wa mwaka 1995 ambapo Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imebainisha haki za wanawake za kushiriki katika maamuzi
Ndio maana chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA kwa upande wa Zanzibar wanao mradi wa miaka minne wa uhamasishaji wa wanawake katika demokrasia na uongozi ambapo lengo lake ni kufikia kiwango cha kuridhisha katika nafasi za uongozi kwa wanawake ifikapo 2020 hadi 2025.
Mradi ambao wanashirikiana na Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar ‘ZAFELA’, PEGAO na watawafikia walengwa wanawake 6,000 kwa Unguja na Pemba.
WANAVYOZUNGUMZA WANAWAKE
Mmoja wa wanawake waliozungumza na makala haya Fatma Jabir wa Mkoani anasema bado wanawake wanaonekana kuwa ni waoga katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Anasema hao wachache wanaotaka kugombea basi hurejeshwa nyuma na wanaume na kupewa vikwazo mbalimbali na hatimae kuvunjika moyo na kukata tamaa.
Kwa hivyo ni vyema wanaharakati wakatilia mkazo katika kuelimisha wanawake kujiingiza kwenye nafasi za uongozi katika uchaguzi ujao 2025.
“Sisi wanawake tusikubali kukaa nyuma nyuma na tusiridhike na nafasi za kuteuliwa pekee, kuanzia sasa tusonge mbele kwanza ukitazama ndio tulio na idadi kubwa ya wapiga kura majimboni”.
Rahma Hafidh wa kijiji cha Konde anasema ili wanawake waweze kuwa na mafanikio katika uchumi, siasa na kijamii ni wakati wa kuamka na kuacha woga katika kugombea nafasi za uongozi.
Anasema mitazamo na dhana potofu zinazojengeka katika jamii hasa katika kugombea nafasi za uongozi kwa mwanamke zinarejesha nyuma kufikia malengo yao.
Arafa Abdi wa Mkaoni anasema tatizo kubwa linalowarejesha nyuma wanawake kugombea nafasi za uongozi ni kukosa ushirikiano na akina baba.
Anasema pamoja na kuwa wanawake hawajakatazwa kuwa viongozi lakini hutumia vipengele mbalimbali ikiwemo cha dini kuwarejesha nyuma wanawake.
“Wanawake tuelewe kuwa dini haijakataza wanawake kuwa viongozi na hasa kwa hizi nafasi za kawaida na wala hoja hiyo tusiitilie maanani,”alisema.
Haroub Juma wa Wete anasema wanawake hawapaswi kukata tamaa ya kugombea nafasi za uongozi kwa kisingizio chochote kile vyenginevyo watabakia kuwa nyuma kila siku.
Anasema mwanamke anapokuwa kiongozi hata neema huongezeka kutokana na imani na huruma waliyonao ni tofauti na wanaume.
Anasema wanawake wengi wamejaaliwa kuwa na uwezo na utambuzi mkubwa hivyo wasijibweteke majumbani watoke na kujikurupua na kupatikana kundi kubwa katika chaguzi zijazo.
Salma Suleiman wa Mkoani anasema ili wanawake waweze kushika nafasi za uongozi la muhimu waweze kuondoa woga ndani ya familia.
WANAHARAKATI
Mwanaharakati Sabah Mussa Said wa Wete anasema uhamasishaji kwa wanawake katika ushiriki wa demokrasia na uongozi unahitajika kwani bado ni waoga .
Anasema wakati umefika wa kuangalia harakati za wanawake zinazobainisha wazi namna mwanamke anavoweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na kiuchumi.
Katika sensa ya mwaka 2012, Zanzibar ilikuwa na jumla ya idadi ya watu 1,300,000 kati ya hao wanawake walikuwa ni sawa na asilimia 51 ya watu wote.
“Pamoja na uwepo wa idadi kubwa ya wanawake bado ushiriki wao katika ulingo wa democrasia na siasa wamekuwa wakitengwa kutokana na mitazamo hasi ya kihistoria au kijamii”, alisema.
Nae Tatu Abdalla Msellemambae ni mwanaharakati wa wanawake, anasema wanawake wana uwezo wakutambua mahitaji ya jamii yao ila ushiriki wao ni mdogo kwenye kutowa maamuzi kutokana na kuwa ni kidogo katika vyombo hivyo.
Anasema miongoni mwa changamoto kubwa inayowakumba wanawake katika vyombo vya maamuzi ni ufinyu wa uwezeshaji na uchache wa ushiriki katika vyombo muhimu vya kutowa maamuzi kwenye jamii na Serikali kwa ujumla.
Maamuzi mengi yamekuwa yakitokea bila ya kuzingatia uhitaji wa mwanamke na ndio maana hupelekea athari katika kuwezesha ustawi na maendeleo ya wanawake na jamii kwa ujumla.
Mwanaharakati Nassour Hakim Haji wa Mkoani anasema tafiti zinaonesha kuwa wanawake wanafanya vizuri katika nafasi za uongozi kutokana na kuwa ni watu wa kutimiza ahadi ,ni watu wa kujitolea , wanaheshimu usawa wa kijinsia na ni waadilifu zaidi.
Anasema katika uchaguzi unaoelekea wa mwaka 2025 ni jambo zuri iwapo wanawake watajitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi maana nao wataweza kushiriki kwa wingi katika kutoa maamuzi.
Anasema wanawake wameleta mafanikio mengi makubwa katika bara la Afrika na duniani kote, mfano Bibi Ellen Johson Sirleaf amekuwa Rais wa kwanza mwanamke Barani Afrika baada ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2005, na ameshika wadhifa huo hadi mwaka 2017.
TAMWA
Ofisa uwezeshaji wa TAMWA Pemba, Asha Mussa Omar, anasema wanawake wengi hushindwa kufikia malengo na kupoteza ndoto zao za kidemokrasia kutokana na changamoto mbali mbali zilizopo katika jamii.
Anasema wanawake muda mrefu walilala katika kuchakarika kugombea nafasi za uongozi na kupelekea kusahaulika kabisa ndio maana wanaume wakapata fursa ya kushika nafasi za uongozi peke yao.
“Ni jukumu la wanawake wenyewe kuwa na kipao mbele kwenye kugombea nafasi za uongozi kwani hakuna sheria wala mikataba iliyomkataza mwanamke kushika nafasi ya uongozi.
Nae Ofisa mawasiliano wa TAMWA Pemba, Gasper Charles anasema wanawake wana haki sawa na wengine mbele ya sheria, ndio maana wamekuwa wakiwashajihisha kuwa viongozi.
Anasema TAMWA tokea miaka ya 2010 wamekuwa wakihamasisha jamii na hasa kundi la wanawake kuona wanatumia haki yao ya kuwa viongozi.
VIONGOZI
Katibu wa Jumuiya ya Maimamu wilaya ya Chakechake, Yussuf Abdalla Ramadhan, anasema kwenye dini ya kiislamu hakujamkataza mwanamke kuwa kiongozi isipokuwa asiyasahau majukumu yake ya msingi.
Anasema tokea enzi ya Mtume Muhammad (S.A.W) mwanamke amekuwa kiongozi bora na hata leo wapo wanawake walio viongozi na wanatimiza majukumu yao vyema.
Kiongozi wa kanisa la RJS Makangale Isack Maganzo Nzilamoshi anasema Bibilia haijamkataza mwanamke asiwe kiongozi ila mfumo dume uliopo ndani ya jamii ndio tatizo.
Anasema ili kuwawezesha wanawake kugombea jukumu lao ni kuwahimiza wanawake kuingia katika mchakato huo.