NA LAYLAT KHALFAN

MAHKAMA ya Rufaa ya Idara Maalum za SMZ, imetakiwa kusimamia ipasavyo mashtaka yanayopelekwa na kutoa maamuzi bila ya hofu ili kuwatendea haki wapiganaji wanaolalamika au kulalamikiwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa mahakama hiyo katika ukumbi wa Ofisi hiyo, Vuga mjini Zanzibar.

Alisema endapo mahkama itashughulikia rufaa zinazowasilishwa na kuzipatia ufumbuzi itasaidia kwa wapiganaji hao kuiamini na kuikubali taasisi hiyo.

Aidha, alifahamisha kuwa, si busara kuona changamoto mbalimbali zinaendelea kujitokeza ndani ya taasisi hiyo na badala yake itende haki.

Waziri Masoud, alisema ipo haja kujenga utaratibu wa kufanyakazi kwa mashirikiano baina ya tume ya utumishi wa Idara maalum na mahkama ya rufaa ili kupunguza kesi ambazo hazina msingi.

“Naamini hakuna hofu katika kusimamia haki lakini kama ipo basi isiendelee kutokuwepo hofu hiyo ili kutoa maamuzi sahihi kwani tukifanya hivi tutakua tumeijengea haki serikali na chombo hichi cha mahakama,” alisema Waziri huyo.

Alisema zipo sheria zinazoongoza chombo hicho, hivyo ni lazima wasimamie katika kutoa haki kwa yale malalamiko yaliyowasilishwa mahakamani hapo.

Aidha, Waziri huyo, aliahidi kutoa mashirikiano juu ya chombo hicho ili kuona linafikiwa lengo lililokusudiwa.

Mwenyekiti wa Mahakama hiyo, Jaji Rabia Hussein Mohamed, alisema atahakikisha anatoa elimu kwa wapiganaji na maafisa ili kutambua uwepo wa mahkama hiyo na jinsi ya kuitumia.

”Tumefikia sehemu nzuri ya kuondoa ucheleweshaji wa kesi ambazo zipo katika mahkama hiyo ambazo zilikuwepo muda mrefu”, alisema.