NA TATU MAKAME
KIJANA aliyedaiwa kumtorosha msichana aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake, amefikishwa katika mahakama ya mkoa Vuga kujibu shitaka linalomkabili.
Aliyepandishwa mahakamani ni Othmani Said Shilumi (21) mkaazi wa Maungani Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.
Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Shamsi Yassin, alisoma kosa la mshitakiwa huyo mbele ya Hakimu Salum Bakari.
Mshitakiwa huyo, alidaiwa kutenda kosa hilo Januari 9 mwaka 2020 majira ya saa 7:30 mchana, huko Fuoni wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.
Mshitakiwa huyo, alidaiwa kutenda kosa la kumuingilia msichana mwenye umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa), ambae yuko chini ya uangalizi wa wazazi wake.
Sambamba na utoroshaji huo, pia alidaiwa kumtorosha tena msichana huyo kutoka Fuoni Michenzani Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja na kumpeleka Pwani mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 113 (1) (a ) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.
Hata hivyo baada ya kusomewa kosa lake mshitakiwa huyo alikana na kuiomba mahakama impatie dhamana, ombi ambalo lilikataliwa kutokana na kuwa makosa hayo hayana dhamana.
Hata hivyo mshitakiwa huyo yupo rumande hadi April 29 kesi yake itakapotajwa tena.