Kwa nini Mzee Karume alipiga marufuku mchezo wa ngumi?

NA MWANTANGA AME

“SIWEZI kukiuka amri ya Baba yangu kuruhusu watu wapigane hata kama ni kiongozi, niliongoza Wizara ya Michezo, namuenzi Baba yangu Mzee Karume, kwa kufuata wasia wake si kumgeuka”

Hayo ni maneno ya Mtoto wa pili wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Balozi Ali Abeid Aman Karume, ambaye katika serikali ya awamu ya saba iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mstaafu, Dk. Ali Mohamed Shein, alikuwa Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo.

Balozi Karume ambaye hivi sasa ni mstaafu katika serikali hiyo, amekuwa akijishughulisha na kazi mbali mbali binafsi, ambapo katika Makala hii anaelezeza namna alivyomuenzi Mzee Karume, alipokuwa madarakani hakutaka kuukataa wasia wa Baba yake, alipokataza mchezo wa ngumi Zanzibar.

Balozi Karume, anasema akiwa mtumishi wa serikali ya Zanzibar, katika nafasi yake hiyo, alikuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kubadili mambo mbali mbali ya kisera na sheria za idara alizokuwa akiziongoza, lakini sio amri hiyo ya Rais wa kwanza, kwani angefanya hivyo angekiuka wasia wa Baba yake.

Alisema akiwa kiongozi katika wizara hiyo alifuatwa na watu wengi wanaopenda mchezo wa ngumi, lakini hakukufuata mawazo yao kwani angefanya hivyo angemgeuka Baba yake.

Alisema alilikataa kwa kukumbuka msemo wa Chama chake cha ASP, kwa wakati huo wa kumuenzi Mzee Karume unaosema, ‘Kilichokufa kiwili wili chake , mawazo na vitendo vyake bado vitakumbukwa’’.

“Mimi nimebahatika kuwa waziri wa Michezo, basi nitilie mkazo kwenye hili, haturudi nyuma hapa Zanzibar hapana ruhusa kupigana ngumi ila wakitaka wakapigane Tanzania bara na kwingine duniani na tunawaomba ”.

Alisema Mzee Karume alipenda mchezo wa mpira wa miguu, bao na dhuna, kiasi ambacho hata kifo chake kilimkuta wakati akicheza mchezo huo na sio gumi.

Alisema Mzee Karume alikataa mchezo huo baada ya kutambua kuwa ni mchezo hatari katika maisha, kwani walioshiriki wengi wao walijikuta wakipata madhara uzeeni.

Alisema michezo mingi ambayo ilikuwa inafanyika ilipata mafanikio na kuipata sifa Zanzibar katika ukanda wa Afrika Mashariki, kiasi ambacho hadi sasa historia yake haijafutika ndani ya miaka hii ya kifo cha Mzee Karume.

Hatua hiyo ya Mzee Karume, Balozi Ali alisema ilikuwa na machungu kwa mabondia waliopenda mchezo huo, kwani haikuwa ajabu kwa Zanzibar kuchukua maamuzi hayo, kutokana na baadhi ya mataifa yaliamua kuzuiya mchezo huo usichezwe.

Alisema mchezo huo pia ulipigwa marufuku nchini Marekani, Macao na Lasverga, waliona ubaya wa mchezo huo na walipenda michezo itayowasaidia katika kuinua uchumi na sio kupigana.

Kutokana na hali hiyo Balozi Karume alisema haishangazi Mzee Karume kuchukua uamuzi huo baada ya kuona kuna ukweli juu ya suala hilo na ndio maana aliamua kupiga marufuku.

“Baba yangu ndie aliyetoa kauli ya kukataza kuchezwa ngumi baada ya kualikwa kwenye pambano la masumbwi ambalo liliandaliwa na raia mmoja wa Ghana, alipofika katika eneo hilo ndipo mzee Karume alipotoa kauli ya marufuku kuchezwa masumbwi” alisema.

“Alipofika pale aliangalia na kuuliza kwanini wanataka kupigana,alipoambiwa ni mchezo wa ndondi akasema mwisho leo, kwa vijana wa Kizanzibari, ‘kupigana masumbwi kufanywa kama watumwa”, alisema Balozi Karume.

Alisema hivi sasa mchezo ulioruhusiwa hapa Zanzibar ni karate ambao ambao ni na gumi.

Katika sera ya michezo mzee Karume alisema vyema kuchezwa michezo yenye maadili, michezo yoyote yenye madhara yanayoonekana na yasiyooneka, michezo hiyo isicheze.

Balozi Karume, anaeleza zaidi kuwa hayati Karume alifikia uamuzi kwa kuzingatia historia ya namna Visiwa vya Zanzibar vilivyopata Uhuru wake kwa Mapinduzi, hivyo kuhusisha kupigana huko kuwa sawa na kuendelea kuwa chini ya wakoloni.

Alisema hivi sasa kumekuwa na mapambano mengi yanayochezwa Tanzania Bara, ya mchezo huo, lakini hakuona nafasi ya kumshawishi kubadili mawazo ya ruhusu vijana wa Zanzibar wapigane ndani ya nchi yao, ambayo imewatafutia uhuru wa kujitawala na sio kuendeleza visasi kwa kupigana ngumi.

Alisema hatua hiyo ilikuwa ni ngumu kueleweka na wapenzi wa mchezo huo, kwani walijaribu kutafuta miadi ya kuonana naye mara kwa mara, lakini hakuweza kubadili msimamo wake wa kuikiuka sera hiyo hadi leo ameondoka madarakani.

MAMA FATMA ALIIPOKEAJE

Mama Fatma Karume, ambaye ni mjane wa Mzee Karume, anasema katika uhai wake alikuwa akipenda michezo lakini masumbwi hakuyapenda na ndio maana aliamua kupiga marufuku.

Mama Fatma anasema anakumbuka siku moja Mzee Karume, aliletewa taarifa ya kualikwa mchezo huo, lakini aliporudi alilalamika sana na kusema huo sio mchezo na hatokubali watoto wa kizanzibari waucheze.

Alisema yeye akiwa na Mzee Karume hakutaka kumshirikisha kwenda kuangalia michezo, lakini alikuwa akishabikia timu baada ya kurudi katika michezo hupewa matokeo.

Ikumbukwe kwamba mchezo wa Masubwi (ndondi) ni moja kati ya michezo mikubwa na yenye umaarufu mkubwa dunia kote, lakini hadi sasa mchezo huu ni marufuku kuchezwa katika visiwani Zanzibar.

Maamuzi haya ya miaka mingi yamekuwa yakiwasumbua mabondia wengi walioko Visiwani Zanzibar, mabondia wanaruhusiwa kufanya mazoezi tuu, lakini kupigana wapigane Tanzania bara au nje ya nchi.

MICHEZO ALIYOWAHI KUSHIRIKI

Mzee Karume katika uhai wake, alijiunga na timu za mpira wa miguu na kujuana na watu mbalimbali.

Kwa wakati huo timu za mpira wa miguu zilizojulikana Unguja zilikuwa ni timu ya skuli ya Kiungani iliyoanzishwa na Mwalimu Augostino Ramadhani na John Majaliwa.

Baadaye kuliundwa timu nyengine za mpira wa miguu ambazo ni Vuga Boys, New Generation, United Service na New Kings.

Karume alijiunga na timu ya New Generation na kucheza nafasi ya mstari mshambuliaji wa pembeni. Baadhi ya waanzilishi wa timu hiyo ni Malingumu, Shaaban Feruzi, Saad Shoka, Masoud Thani na Mzee wa Shangani.

Mara tu baada ya kujiunga na timu hiyo, Karume alichaguliwa kuwa msaidizi nahodha.

Katika mwaka 1920 Abeid Amani Karume alikubaliwa kuwa baharia katika meli iliyoitwa Golden Crown (Taji la Dhahabu), jambo ambalo lilimpunguzia kuendelea na michezo kwani Meli hiyo ilichukua abiria na mizigo kati ya bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam, Pemba, Tanga, Mombasa na Mikindani huko Kilwa jambo ambalo lilimyima muda kuendelea na michezo.