NA ASYA HASSAN
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), ACP Ahmed Khamis Makarani, amewataka wafanyakazi wa Mamlaka hiyo wasibweteke na badala yake kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, ili waweze kuleta ufanisi ndani ya mamlaka hiyo.
ACP Ahmed, alisema hayo katika ukumbi wa ZAECA, uliyopo Victoria Garden, alipokuwa akijitambulisha kwa watendaji na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia kwenda sambamba na malengo ya serikali ya kudhibiti vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi hapa nchini.
Alisema ili kudhibiti vitendo hivyo ni vyema wafanyakazi hao kuwa tayari kutekeleza majukumu yao kwa uweledi na kuacha nidhamu ya woga.
Mkurugenzi huyo, alisema endapo kila mfanyakazi akitumia nafasi yake ipasavyo katika kutekeleza majukumu yake basi itakuwa chachu ya kupambana na vitendo hivyo na kuleta maendeleo mapana ndani ya taifa.
Kuhusu utendaji wa kazi Ahmed, alisema suala hilo linahitaji ushirikiano na utendaji bora kwa kila mtu kujituma na kutekeleza majukumu yake, hatua ambayo itasaidia kuleta maendeleo ya pamoja juu ya kupambana na vitendo hivyo.
“Kila mtu lazima atambue kwamba anawajibu wa kufanikisha malengo ya serikali juu ya kupambana na kudhibiti vitendo hivyo,”alisema.
Watendaji hao waliahidi kushirikiana na kiongozi huyo pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, ili kuleta matunda chanya kwa jamii na serikali kwa ujumla.