NA MWANDISHI WETU
MAMENEJA Biashara wa Mamlaka za Maji Nchini wamesisitizwa kuweka mikakati madhubuti ya ukusanyaji wa mapato, ili kuboresha na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa wananchi wa maeneo yao ya huduma.
Wito huo umetolewa Jijini Mwanza na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, wakati wa ufunguzi wa mkutano uliokutanisha Mameneja Biashara wa Mamlaka zote za Maji nchini.
“Suala la mauzo na mapato yaani makusanyo kwa ujumla tunawategemea nyinyi, ni muhimu mkatambua bila makusanyo mazuri Mamlaka za Maji hazitoweza kujiendesha,” alisisitiza Mhandisi Msenyele.
Mhandisi Msenyele, alisema changamoto miongoni mwa mamlaka za maji nyingi zinafanana ikiwemo ya uwepo wa wadaiwa sugu na upotevu wa maji, na ni vyema kuweka njia bora ya kukabiliana nazo kwa lengo zima la kuhakikisha huduma ya maji inaimarika.
“Mtakachojadili na kujifunza hapa mkichukulie kwa umuhimu wake na mtakaporudi kwenye taasisi zenu mhakikishe mnazifanyia kazi, ili kupatikane tija iliyokusudiwa,” alielekeza Mhandisi Msenyele.
Meck Manyama, Meneja Biashara kutoka MWAUWASA alisema kikwazo kikubwa wanachokabiliana nacho katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ni uwepo wa wadaiwa sugu waliositishiwa huduma ya maji muda mrefu, lakini hawajajitokeza kulipa madeni yao.
“Hawa wadaiwa sugu wanatukwamisha kuboresha huduma, sisi hatuna ruzuku tunajiendesha kwa fedha zitokanazo na malipo ya ankara za maji ili kulipia umeme, kununua dawa na kukarabati miundombinu sasa inavyotokea baadhi ya wateja kushindwa kulipa inatuwia ngumu kuboresha huduma,” alifafanua Manyama.
Naye Meneja Biashara kutoka Mamlaka ya Maji ya Dodoma (DUWASA), Alex Mpagama alibainisha kwamba mamlaka inadai wateja wake zaidi ya shilingi bilioni 1.7 fedha ambayo ilipaswa kutumika kuboresha huduma kwa wakazi wa Dodoma.
Hata hivyo, alibainisha kwamba tayari baadhi ya wateja wameanza kupunguza madeni yao kwa kuyalipa kwa awamu na alisisitiza wengine kulipa, ili kuipa nguvu DUWASA ya kuboresha hali ya upatiknaji wa huduma ya maji.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo kwa ujumla wake, Mwenyekiti wa Mameneja Biashara ambaye ni Meneja Biashara kutoka Mamlaka ya Maji ya Tabora (TUWASA), Biswalo Benard, alisema lengo la mkutano huo ni kujadili changamoto zinazowakabili na kubadilishana uzoefu wa namna ya kupambana nazo.