NA ASIA MWALIM
WAFANYABIASHARA wanaotumia gari (keri) kuuza bidhaa mbalimbali ikiwemo nguo na vyakula wametakiwa kuondoka kando ya barabara na kuhamia maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya biashara, ili waweze kuendesha biashara hizo kihalali.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango, Utawala na Fedha Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi ‘B’, Ameir Ali Haji, aliyasema hayo alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Mchina mwisho Unguja.
Alisema wafanyabiashara wa Wilaya hiyo, wanapaswa kufuata maelekezo yanayotolewa na serekali kupitia viongozi wake, kwa kuhamia eneo la Kijitoupele ambalo limeandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya wafanyabiashara wa aina hiyo.
Aidha, alisema pembezoni mwa barabara haitakiwi kueka gari, na kuigeuza sehemu ya duka kuuza bidhaa, hivyo wanatakiwa kuondoka maeneo hayo na kutumia eneo walilopangiwa kutumia.
Alisema ni vyema biashara zinazoanzishwa nchini kufuata maagizo yaliyoweka na Serikali, ili kuepusha mivutano isiyokua ya lazima sambamba na kupelekea uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar.
Aidha, alisema ingawa kuna mabadiliko yanayoendana na wakati kwenye masuala ya biashara, lakini utaratibu huo sio rasmi, hivyo wanapaswa kufuata utaratibu mzuri kwenye mamlaka zinazohusika.
Alisema kadiri siku zinavyokwenda kulingana na mabadiliko ya kisayansi nchini, wafanyabiashara wanaibua mbinu mpya za kutaka kuwafikia wateja kwa urahisi, ingawa njia nyengine sio sahihi, utaratibu wa serikali.
Alieleza kuwa mara nyingi maeneo wanayotumia sio rasmi, ambapo mara nyingi husababisha ajali kutokana na msongamano wa watu, jambo ambalo linahatarisha usalama kwa watu wa maeneo hayo.
Alifahamisha kuwa kutokua na sehemu husika ya kufanyia biashara hizo kwa baadhi ya watu kunaikosesha Serikali mapato yake, jambo ambalo linajeresha nyuma maendeleo ya wananchi na Taifa kiujumla.
Aidha, alisema licha ya kuwa biashara zinatoa mahitaji ya mtu ya kila siku, lakini inapaswa kuzingatia vitu muhimu ikiwemo kufata ushauri ili kupewa uhalali wa kuendelea na biashara zao .
Mapema Mkurugenzi huyo alieleza kuwa baraza hilo limefanya jitihada za kufatilia maeneo hayo, ili kuona utaratibu mzuri unatumika kwa watu hao ikiwemo kuweza kulipa kodi, hivyo wameandaa eneo la Kijitoupele ambalo linauwezo wa kukusanya gari (keri) zote.
Alieleza kuwa eneo hilo litatumika kwa muda, ambapo uongozi huo ukiendelea kuandaa mikakati ya kuweka eneo rasmi litakalo tumiwa kwa ajili biashara zinazouzwa kwenye keri.
Sambamba na hayo alihimiza kuzingatia uimarishwaji wa mazingira kwenye biashara zao kwa kuziweka katika hali ya usafi, ili kuendelea huhamasisha wateja na kujiengezea wateja wapya.
“Kwenye suala la biashara usafi ni kipaombele cha wateja wengi ambao wanategemewa kununua biashara hizo ili kuweza kupata hizo faida wanazozitaka” alisema.