NA VICTORIA GODFREY

WADAU wa Mpira wa Kikapu mkoani Manyara wametakiwa kujitokeza kuthibitisha kushiriki mafunzo ya ukocha na uamuazi ambayo imepangwa kuanza Aprili 23- 29 kwenye viwanja vya Kwaraa Bahati mkoani humo.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Chama cha Mpira wa Kikapu mkoa na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF).

Ofisa michezo wa mkoa wa Manyara Charles Maguzu,alisema uthibitisho huo utaenda sambamba na ulipaji wa ada ya ushiriki.

Alisema lengo ni kuwajengea uwezo makocha na waamuzi ambapo badaye watakuwa na jukumu la kufundisha na kusimamia mchezo huo ndani na nje ya mkoa.

” Tunahitaji kuhakikisha tutapata walimu na waamuzi wa kutosha ambazo watakuwa na jukumu la kuinua na kuibua vipaji vya Vijana wetu kuanzia ngazi ya chini hadi juu na pia kuleta maendeleo ya michezo ndani ya mkoa wetu,” alisema Maguzu.

Maguzu alisema mkufunzi wa mafunzo hayo ni Alfred Ngalaliji.