NA KHAMISUU ABDALLAH

TUME ya kurekebisha sheria Zanzibar, imesemamarekebisho ya sheria na sera ya ardhi, yatasaidia kuondoa migogoro ya ardhi hapa Zanzibar na kuimarisjha ustawi wa jamii.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Khadija Shamte Mzee, wakati akifungua mkutano wa siku moja ulioshirikisha taasisi mbali mbali za umma zinazohusika na masuala ya ardhi uliofanyika katika ukumbi wa mdogo wa mikutano wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani.

Alisema, hatua hiyo itasaidia upatakanaji wa sheria ambazo zitakwenda sambamba katika kuweka utaratibu mzuri wa umiliki wa ardhi na kumpa moyo mtu kuamini katika umiliki huo.

Aidha alisema sheria za ardhi zinawagusa moja kwa moja wananchi na maeneo ya kiuchumi ambayo yanategemewa katika kukuza pato la taifa. 

Alisema, wameamua kuwaita wadau wa masuala ya ardhi kutokana na kuongezeka kwa migogoro mingi ya ardhi kila siku bila ya kupatiwa ufumbuzi.

“Kama tume baada ya kupitia sheria za ardhi tumeona sio busara kuzitia mkono zote kwa ujumla wake ili tusije tukaharibu, ndio maana tumewaita ili kupata maoni,” alibainisha Mwenyekiti huyo.

Aidha Khadija, alisema dhamira ya tume ni kusikia changamoto zilizopo katika katika sheria hizo ili kuona matatizo ya msingi yanayokwaza utekelezaji wa majukumu yao.

“Mambo ya ardhi kila siku yanabadilika sheria ya ardhi zinabadilika kwani hayasimami pekee yake, inashirikisha serkta mbali mbali ikiwemo kilimo, utalii, makaazi ya watu na hata uchumi,” alisema.

Akizungumzia lengo la mkutano huo alisema ni kuiwezesha sera ili kuitizama kama inakidhi mahitaji ya sasa na inakwenda na mabadiliko ya sasa au tofauti.

Alisema wadau hao ni muhimu kwani ndio watendaji wakuu wa tasisi zinazoshughulikia ardhi na malalamiko mengi yanayolalamikiwa na wananchi yanatokana na watendaji wa tasisi za serikali katika utaratibu wa kuwahudumia wananchi.

Aidha alifahamisha kuwa wakiweza kuweka taratibu vizuri basi itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya ardhi iliyokuwepo nchini.

Alisema wamebaini suala la ardhi katika kazi na majukumu linaonesha kila mamlaka ina uwezo na kuwa na kazi nyingi hali ambayo inawahangaisha wananchi.

Hivyo alisema upo umuhimu wa kuweka utaratibu maalum ambao utamuwezesha mwananchi kupata huduma nzuri na kuwapa elimu katika suala la ardhi na umiliki wake.

Nae, Katibu wa Tume hiyo, Mussa Kombo, alisema mkutano huo umeshirikisha watu muhimu ambao watasaidia kuondosha migongano ambayo ipo na itakayoweza kujitokeza katika sheria mbalimbali za ardhi na kushirikiana katika kuondosha changamoto za kisheria zilizopo au za kiutendaji.

Nao wadau walioshiriki katika mkutano huo walisema sheria nyingi haziendani na wakati uliopo na zinamgongano baina ya tasisi na taasisi.

Dk. Abdulnassir Hikmany, kutoka ofisi ya Mrajis wa ardhi, alisema uhaba wa wataalamu unapelekea kuchelewa kwa upatikanaji wa hati za umiliki wa ardhi kwa wananchi.

Nae, Mtendaji kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, Assa Jaffar Omar, alisema kuwepo kwa taasisi nyingi zinazohusika na masuala ya ardhi inapelekea kuingiliana katika utendaji hivyo ipo haja ya kubadilisha sheria na kuweka tasisi moja itakayoratibu masuala hayo.