NA ASYA HASSAN
WAKAAZI wa Shehia ya Matemwe wameiomba serikali kuangalia upya mfumo wa ajira unaotolewa ndani ya mahoteli ya kitalii kutokana na asilimia kubwa ya hoteli hizo haziwaangalii wazawa.
Wananchi hao walisema hayo walipokuwa wakitoa kero zao mbele ya maofisa wa ZAECA walipokuwa wakipatiwa elimu juu ya masuala ya udhalilishaji na madhara ya rushwa hafla ambayo ilifanyika katika Skuli ya Sekondari Matemwe Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Walisema asilimia kubwa ya wananchi waliyopo ndani ya vijiji hivyo hawanufaiki na ajira za mahoteli kutokana na wamiliki wa hoteli hizo kuwapa kipaumbele wananchi kutoka nje na sio wazawa.
Walifahamisha kwamba hali hiyo huwafanya wananchi wengi waliyopo ndani ya maeneo hayo hususani vijana kukosa ajira, na badala yake kubakia katika kufanya kazi za kuuza unga.
Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Juma Haji Juma, alisema licha ya kutoa maeneo yao kwa ajili ya uwekezaji lakini bado kumekuwa na urasimu na kuwafanya wakaaz hao kutonufaika nalo.
“Nivyema serikali ikatia mkono wake ili ajira zipewe kipaumbele kwa wananchi kupitia kwa masheha wa Shehia za wa shehia husika ili kuweza kufaidika nazo,”alisema.
Wakizungumzia kuhusu kituo cha afya wananchi hao waliiomba serikali kuwawekea utaratibu mzuri, ili kituo hicho kiweze kufanya kazi masaa 24.
Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Makame Bakari Haji, alisema wamekuwa wakisumbuka pale wanapopata mgonjwa nyakati za jioni au usiku hushindwa kupata huduma hadi waende hospitali ya Kivunge.
Walisema jambo hilo huwawia vigumu na kuchangia kurudisha nyuma maendeleo yao.
Wakizungumzia kesi za udhalilishaji walisema masuala hayo bado yanaendelea kutokea na sababu kubwa ni baadhi ya wazazi na walezi huendelea kuyafumbia macho.
Kwa upande wa Ofisa kutoka ZAECA Sada Salum Issa, akitolea ufafanuzi suala la udhalilishaji alisema serikali imeanzisha mahakama maalum ya kushulikia suala hilo hivyo ni vyema wananchi kuunga mkono jitihada hizo ili kutokomeza vitendo hivyo.