NA MADINA ISSA

KAMISHNA wa Kazi, Fatma Iddi Ali, amewataka mawakala binafsi za ajira nchini kuzingatia sheria zilizopo zinazohusu shughuli hiyo ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.

Akifungua mkutano wa siku moja wa kuzijengea uwezo taasisi binafsi za ajira kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mussa Haji Ali hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji uliopo Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Alisema, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji haitavumilia taasisi yoyote itakayo kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa kisheria katika shughuli za wakala binafsi za ajira.

Alisema wakala binafsi wa ajira wamepewa ruhusa kisheria kuwaunganisha waajiri na watafuta kazi kote duniani, hivyo katika kuendesha shughuli hizo wahakikishe wanakuwa na taarifa za waajiri.

Katibu mkuu huyo aliwasisitiza kupeleka wananchi wenye elimu ya kujitambua, ujuzi na uwezo wa kazi badala ya kuchukua yoyote, kufuatilia taarifa za watu waliosafirishwa na kutoa taarifa haraka linapotokea tatizo.

“Msifanye kazi kwa tamaa jalini kuwa hii ni kazi rasmi inayotambuliwa na serikali, hakikisheni mnakidhi masharti na maelekezo ya sheria na kanuni pamoja na kushirikiana na balozi zetu za Tanzania zilizopo nje ya nchi”, alisema.

Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafahamu umuhimu wa taasisi hizo za wakala binafsi wa ajira na inathamini jitihada zao kwani inasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Nae Kaimu Mkurugenzi Idara ya ajira ambae ni Mkurugenzi Idara ya Usalama kazini, Suleiman Khamis Ali, alisema tangu utaratibu wa wakala wa ajira kuanza kazi mwaka 2012 ajira 8,1161zimepatikana nje ya nchi.

Kwa upande wa mawakala wameomba idara ya ajira na kamisheni ya kazi kuzungumza na waajiri binafsi wakiwemo waekezaji kwani inaonekana dhana ya kuwepo mawakala wa ajira hawajaifahamu.

Sambamba na hayo, walisema watajitahidi kushirikiana na nchi mbalimbali duniani na wamezipongeza nchi za Kuwait na Qatar kwa ushirikiano wao ambao unawezesha kuwepo ufanisi wa kazi yao.