MOGADISHU, SOMALIA

SOMALIA imesema kuwa mazungumzo kati ya serikali ya nchi hiyo na viongozi watano wa majimbo nchini humo yataendelea.

Ofisi ya mawasiliano ya ikulu imesema, mazungumzo yaliyoanza Aprili 3 mwaka huu kati ya serikali na viongozi wa majimbo ya Galmudug, Hirshabelle, Puntland, Jubaland na Southwest yatasitishwa kutokana na kutokuwepo kiongozi mmoja.

Taarifa zaidi zilizotelewa na serikali ni kwamba mazungumzo hayo yataendelea baada ya kiongozi aliyeshindwa kuhudhuria kuthibitisha kuwa yupo tayari kushiriki kwenye mazungumzo hayo.

Awali viongozi wa majimbo ya Hirshabelle, Puntland, Jubaland na Southwest walihudhuria kwenye mkutano uliomashirikisha rais wa nchi hiyo, lakini kiongozi wa jimbo la Galmudug hakuhudhuria.

Mazungumzo hayo ambayo yamekuwa yakifanyika mjini Mogadishu yatakamilisha utekelezaji wa mfumo wa uchaguzi, juu ya msingi wa kazi ya kamati ya ufundi iliyofanyika Baidoa katika mkoa wa Kusini Magharibi.

Somalia imejikuta kwenye mkwamo wa kisiasa baada ya kushindwa kufanya uchaguzi mkuu na hivyo rais Mohamed Abdullahi Farmaajo kuendelea kuwa madarakani.

Kutokana na hali hiyo vyama vya upinzani vinapinga rais Mohamed Abdullahi Farmaajo kuendelea kuwa madarakani huku vikimshutumu kwa kushindwa kusimamia kufanywa kwa uchaguzi ili aendelee kubakia madarakani.