Asema ataunyoosha muungano
NA SAIDA ISSA, DODOMA
MBUNGE wa Viti maalum Zanzibar, Asya Mwadini Mohamed ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kuuheshimisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuzigawa fedha za maadhimisho ya muungano pande zote mbili.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuelekeza fedha zilizotengwa kwenye maadhimisho ya siku ya muungano kugawanywa pande mbili jambo linalodhihirisha serikali ina nia ya dhati kuudumisha na kuuhifadhi muungano.
Hayo aliyasema mbunge huyo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya muungano jijini Dodoma ambapo alisema kuwa hatua hiyo imewatia moyo wazanzibari kwa ujumla.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuishauri serikali kuweka mambo sawa yanayohusu mfuko wa pamoja wa muungano ikiwa ni pamoja na kuweka uwazi wà mgawanyo kwa pande zote mbili za muungano.
“Tunaomba mfuko huu uwekwe wazi na kujadiliwa hapa, tunataka tuone kipengele kinachouchambua mfuko huu ili kuwepa mambo sawa kuanzia kiasi kilichopo na mgawanyo wake, haya yote yakiwekwa wazi itasaidia kupunguza kelele za mitaani,”alisisitiza mbunge huyo.
Asya aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuimarisha mahusiano ya kidemokrasia kwa kumpa nafasi Rais wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kumuwakilisha kwenye mkutano wa nchi za SADC.
“Hatua hii imetupa faraja sana, na ninampongeza sana na sasa tunaona kweli muungano unakwenda kuwa safi kwa kuzingatia haki bila upendeleo,”alisema.
Licha ya hayo, Asya alisema pamoja na mazuri ambayo yameanza, bado serikali inapaswa kuboresha masuala kadhaa ambayo yanazungumzwa kama kero za muungano.
Katika hatua nyingine, akichangia kipengele cha mazingira, alisema serikali ilitoa tamko la uzuiaji wa mifuko ya plastiki nchini iliyoonekana kikwazo katika uhifadhi wa mazingira lakini cha kushangaza baadhi ya wafanyàbiashara bado wanaendelea kutumia na watu wanaendelea kuitumia jambo linalotia hofu kwa ulinzi wa mazingira.
Pamoja na hayo Asya alizungumzia kuhusu ufuatiliaji wa mafao kwa wastaafu ambapo aliishauri serikali kuona namna ya kuboresha mifumo iliyopo ili kuwasaidia kuondokana na usumbufu wanaoupata.