NA TATU MAKAME

MBUNGE wa Jimbo la Bububu, Mwantakaje Haji Juma, amewahakikishia wananchi wa Kijichi Kitongoji cha Mshikemshike kuwa huduma ya maji safi na salama inayowakabili itaondoka.

Mbunge huyo alisema hayo Jimboni Bububu Wilaya ya Magharibi ‘A’, wakati alipokuwa akisikiliza kero za wananchi ikiwa ni muendelezo wa ziara za kusikiliza kero zao.

Hata hivyo, Mbunge huyo alitoa msaada wa shilingi 500,000 kwa ajili ya kufanyiwa usafi kisima kilichopo Kijichi Mshikemshike, ili kuwaondoshea kero ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama wananchi wa eneo hilo.

Alisema huduma ya maji ni muhimu kwa kila kiumbe hai hivyo aliwahakikishia wananchi kuwa tatizo hilo litaondoka siku chache.

 “Mchimbaji wa kisima huwa anaendeleza sadakataul -jaria hivyo na sisi viongozi tunawajibu wa kutekeleza hilo, kwani tuliweka ahadi kwa wananchi wetu kuwaondoshea kero zinazowakabili”, alisema.

Aliwataka wananchi kuendelea kukitunza kisima kitumike muda mrefu pamoja na kuwataka kuacha kufanya israfu kwa kuharibu miundombinu ya maji.

Diwani wa Wadi ya Bububu, Ramadhani Juma Mkanga, aliwataka wananchi kuthamini juhudi zinazochukuliwa na viongozi wa majimbo za kutatua kero za wananchi na kwamba atafuatilia matatizo na kero zinazowakabili wananchi pale wanapoona kuna haja ya kufanya hivyo.

Alisema kisima hicho kilichimbwana na wananchi wenyewe ila wameshindwa kukifanyia usafi hivyo kutolewa kwa fedha hizo kutarahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi mara watakapomaliza kufanya usafi.

 Katibu wa CCM Jimbo la Bububu, Zaituni Khairalla Tawakala, alisema kazi kubwa inayofanya na viongzi wa majimbo ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hivyo aliwanasihi viongozi wa majimbo kuendelea kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi.

Mapema wakizungu na Mwandishi wa Habari, wananchi wa shehia ya Kijichi kitongoji cha Mshikemshike walisema wametumia zaidi ya shilingi 3,000,000 kwa ajili ya uchimbaji wa kisima pamoja na ununuzi wa tangi la kuhifadhia maji, lakini wameshindwa kukifanyia usafi kutokana na kujaa kwa michanga ndani ya kisima.

Hata hivyo, walimshukuru Mbunge huyo kwa kuweza kuwapatia fedha hizo na kumtaka kuwa karibu kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi.