NA HUSNA SHEHA
VIONGOZI wa Jimbo la Mtoni wamewataka wananchi wa jimbo hilo kuhakikisha wanaweka mazingira safi hasa katika kipindi hichi cha mvua zinazoendelea kunyesha.
Mbunge wa Jimbo hilo, Abdulghafar Idrissa Juma, alitoa kauli hiyo katika hafla ya kukabidhi vifaa vya usafi kwa shehia tatu vilivyotolewa na viongozi wa jimbo hilo huko Kibweni.
Alisema ni wakati sasa wananchi kubadili tabia zao kwa kusafisha mazingira yanayowazunguka mara kwa mara, ili kujiepusha na maradhi mbalimbali hasa ya mripuko.
Aidha alisema imezoeleka inapofika kipindi cha mvua hasa za masika maradhi ya kuharisha yamekuwa yakijitokeza hivyo ni wakati wao kutoyapa nafasi.
Alisema wamekuwa wakichukua jitihada mbalimbali kuhakikisha wanawaletea maendeleo wananchi, kwani ndio waliowapa ridhaa katika uchaguzi mkuu wa 2020.
“Tunajitahidi katika vikao vyetu vya Bunge, Baraza la Wawakilishi na Madiwani, ili tuweze kupata fedha za jimbo ambazo zitaweza kuwasaidia nyinyi wananchi wetu kwa kuwatatulia kero mbalimbali zinazowakwanza,” alisema.
Hata hivyo, alibainisha kuwa kwa kushirikiana pamoja watahakikisha wananchi wanapata maendeleo hatua kwa hatua ili kufikia lengo walilokusudia kisiasa na kijamii.
Aliwataka wananchi kuvitumia vifaa hivyo kwa lengo lilokusudiwa ikiwemo la kuweka jimbo lao katika hali ya usafi.
Mwakilishi wa jimbo hilo Hussein Ibrahim Makungu aliahidi kushirikiana na viongozi wenzake ili kuhakikisha jimbo hilo linakuwa na maendeleo ya kupigiwa mfano.
Nao wananchi wa jimbo hilo waliwapongeza viongozi wao na kuelekeza kuwa bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo ya maji.
Changamoto nyengine, walisema ni ushirikiano mdogo kwa viongozi hasa kwa wananchi walioanzisha vikundi mbali mbali vya kisiasa na kijamii kutowapitia na kujua kero zao hali ambayo inawarejesha chuma.
Hivyo, waliwaomba viongozi hao kuwachimbia kisima ambacho kitaweza kuondosha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama hasa katika kipindi hichi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Miongoni wa vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na gari moja aina ya keri, mabero 15, mapauro, viatu, glavzi, Maski, reki pamoja na hundi ya shilingi 500,000 kwa kikundi cha usafi cha shehia ya Kibweni kwa jitihada nzuri wanayoifanya katika suala la usafi.