NA JOSEPH DAVID

MENEJA wa mshambuliaji wa kimataifa wa Simba na nyota wa timu ya Taifa ya Rwanda Meddie Kagere, Patrick Gakumba ‘Super Manager’, ametamba kuwa uwezo wa mchezaji wake kufumania nyavu bado upo juu.

Akizungumza kwa njia ya simu kupitia kipindi cha michezo kutoka kituo cha Clouds Fm mara baada ya mechi ya Simba na Mtibwa Sugar wiki iliyopita, Gakumba alibainisha kuwa uwezo wa Kagere anaujua hivyo kutokufunga mechi kadhaa zilizopita ulikuwa ni upepo wa muda mfupi tu, hali ambayo inaweza ikamtokea mchezaji yeyote.

“Waliokuwa wanambeza Kagere leo amewazodoa kwa kuweka nyavuni mabao mawili, hali kama hii iliwahi kumtokea hata msimu uliopita lakini mwisho wa msimu akaibuka kuwa mfungaji bora wa ligi,”alisema Gagumba.

Meneja huyo alisema mchezaji wake amekuwa na kiwango bora toka akicheza timu ya APR, Gormahia na hatimaye Simba na amekuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa misimu miwili mfululizo.

Gakumba aliendelea kusema hajawahi kuwa na mashaka na kiwango cha Meddie Kagere hata kidogo, kwani hamna mchezaji yeyote barani Afrika aliyefikia rekodi ya Kagere kuwa mfungaji bora wa ligi tatu tofauti.

Sambamba na hayo meneja huyo alisema ana imani kubwa na mchezaji wake kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa ligi kuu ya Tanzania bara kwani baada ya kukaa miezi kadhaa bila kufunga karudi kwa kishindo na kumshusha Prince Dube wa Azam Fc kwenye kilele cha upachikaji mabao.

Aidha Gakumba ameipa pongezi Simba kwa kufanya vizuri kwenye mashindano ya michuano ya klabu bingwa Afrika na kuitabiria kufika mbali huku akitanabaisha kuwa Simba imechukua nafasi ya TP Mazembe kwenye michuano hiyo.

Meddie Kagere ndiye kinara wa mabao kwenye ligi kuu Tanzania Bara kwa kufunga jumla ya mabao 11 akifuatiwa na Prince Dube wa Azam FC mwenye mabao 10.