NA JUMA SHAALI, JKU

MKUU mpya wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Makame Abdalla Daima amewataka maofisa na wapiganaji wa jeshi hilo kuongeza mashirikiano ili jeshi hilo liweze kufikia ufanisi.

Kanali Makame alieleza hayo jana alipokua akikabidhiwa ofisi pamoja na nyaraka mbalimbali kutoka kwa aliyekua mkuu wa jeshi hilo Kanali Ali Mtumweni Hamadi, hafla iliyofanyika makao makuu ya JKU, Saateni mjini Zanzibar.

Mkuu huyo alifahamisha kuwa Jeshi hilo litapiga hatua za haraka za maendeleo na kuyafikia malengo na matarajio yaliyowekwa endapo maofisa na wapiganaji watakuwa kitu kimoja na kuzidisha ushirikiano baina yao.

“Siri ya mafanikio katika jeshi lolote ni mashirikiano, tukiwa na mashirikiano ya pamoja tutaweza kuyafikia malengo na kupata maendeleo kwa haraka, lazima maofisa na wapiganaji tuwe na mashirikiano”, alisema Kanali Makame.

Kanali huyo aliitaka kamati ya uongozi ya JKU kusimamia vyema matumizi na mapato ya ndani ya jeshi hilo na kwamba wahakikishe wanazuia matumizi yasiyo ya lazima.

Agizo jengine alilolitoa mkuu huyo kwa maofisa na wapiganaji wa jeshi hilo ni kuhakikisha wanatunza nidhamu na utiifu jeshini jambo ambalo litakuza ufanisi wa majukumu yao.

Hata hivyo, aliahidi kusimamia maslahi ya askari wa jeshi hilo kwa kuwapatia stahiki zao mbalimbali na kuwataka kuepuka kufanyakazi kwa mazoea.

Kwa upande wake aliyekuwa mkuu wa JKU, Kanali Ali Mtumweni Hamadi alimuhakikishia mkuu huyo kumpa mashirikiano na kumtaka kusimamia vyema mipaka ya kambi za JKU ili kupunguza migogoro kutoka kwa wananchi.

Hata hivyo aliwataka maofisa na wapiganaji kutunza siri za serikali pamoja na kuongeza kasi ya uzalishaji ili kukuza maendeleo ya jeshi na serikali kwa ujumla.

Makabidhiano hayo yamefanyika kufuatia hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kutengua uteuzi wa Kanali Mtumweni na Kumteua na kumuapisha Kanali Makame kuwa mkuu mpya wa jeshi hilo.