NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa kikosi cha Namungo FC, Hemedi Moroko amesema licha ya machofu walikuwa nayo lakini watapambana ili kuifunga Polisi Tanzania.

Namungo wametoka kucheza mchezo wa kimataifa dhidi ya Nkana FC ya Zambia na kupoteza kwa bao 1-0.

Jana wameingia Mkoani Kilimanjaro na kesho wanatarajia kushuka dimbani kuvaana na Polisi Tanzania kwenye uwanja wa Ushirika.

Akizungumza na Zanzibar Leo,Moroko alisema wamefika jana na wamechoka lakini watapambana kupata matokeo mazuri.

Alisema watatumia siku moja waliyonayo kujiandaa kwani Polisi sio timu ngeni kwao, hivyo watajua jinsi ya kuwadhiti japokuwa haitakuwa rahisi.

“Ndio tumeingia Moshi jana, lakini tumechoka sana kutokana na michezo tuliocheza, lakini sio shida tutapambana kiume kupata matokeo,” alisema.

Mchezo wao wa kwanza Namungo wakiwa wenyeji Polisi Tanzania walipata ushindi wa bao 1-0.

Namungo wanashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 28 huku wapinzani wao Polisi wakiwa nafasi ya nane.