NA MARYAM HASSAN
MSHITAKIWA Omar Mwalimu Fumu (30) mkaazi wa Unguja Ukuu, ameiomba mahakama kumpangia tarehe fupi kwa sababu ana maradhi ya kuanguka.
Ombi hilo amelitoa mbele ya Hakimu Saidi Hemed Khalfan, wakati mshitakiwa huyo alipofikishwa katika mahakama ya mkoa Mwera ajili ya kusikilizwa ushahidi.
Aidha alisema pia hana mtu wa kumchukulia dhamana, hivyo mahakama izingatie kupanga tarehe fupi ili kesi hiyo imalizike haraka.
Omar anakabiliwa natuhuma za kuvunja nyumba kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi, kosa ambalo ni kosa kisheria.
Wakati anatoa maelezo hayo, upande wa mashitaka wa serikali ulikuwa ukisimamiwa na wakili kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Shumbana Mbwana.
Wakili huyo, alikubali ombi la mshitakiwa na kuiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupanga tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.
Kosa la kuvunja, mshitakiwa anadaiwa kutenda Febuari 8 mwaka jana majira ya saa 6:00 za usiku huko Unguja Ukuu wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.
Mshitakiwa anadaiwa kuvunja nyumba aliyokuwa anaishi Joseph Fedrick Buadalia kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi ndani humo, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Aidha mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa la wizi, ambapo anadaiwa kuiba simu aina ya Tecno ya batan rangi ya Silver yenye thamani ya shilingi 45,000 pamoja na fedha taslimu shilingi 40,000 mali ya Joseph Fedrick Buadalia, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Said aliahirisha shauri hilo hadi Aprili 12 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.