NA GASPARY CHARLES
WAKAAZI wa shehia ya Mtambwe kaskazini wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, wamesema inawezekana adhabu ndogo inayotolewa kwa washtakiwa wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ndio chanzo cha vitendo hivyo kuendelea kuongezeka na kusababisha athari zaidi katika jamii.
Waliyabainisha hayo wakati wa mkutano wa kamati ya kupinga udhalilishaji wilaya ya Wete wenye lengo la kuihamasisha jamii kupinga udhalilishaji wa kijinsia.
Othman Haji Kibano akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA Zanzibar) alisema licha ya juhudi zinazochukuliwa na jamii kuripoti taarifa za matukio hayo, bado hukumu zinazotolewa kwa wakosaji zinawakatisha tamaa na kusababisha vitendo vya udhalilishaji kuendelea.
“Tunajitahidi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za vitendo hivi lakini tukimpeleka mtuhumiwa polisi na baadae mahakamani cha kushangaza hukumu anayopata inakuwa ndogo na wakati mwengine anaachiwa akiwa kituo cha polisi. Hii inatuvunja moyo kwani sisi ndio tunaoumia huku mtaani,” alisema.
Nae Hamad Idd Hamad, alisema kama kweli serikali inataka vitendo hivyo vimalizike katika jamii basi washitakiwa wasiachiwe huru na wapewe adhabu kulingana na uzito wa makosa waliyotenda.
Alisema kutokana na watuhumiwa kuachiwa huru husababisha baadhi yao kuchukua sheria mikononi ikiwemo kuwashambulia pale wanapowabaini wanafanya vitendo hivyo.
Mapema Ofisa ustawi wa jamii wilaya ya Wete, Haroub Suleiman Hemed, alisema jamii haipaswi kukata tamaa juu ya utoaji taarifa za vitendo hivyo kwani kufanya hivyo kutazidi kuwapa nguvu watuhumiwa.
“Watu wengi wanadhani kwamba njia sahihi baada ya kutokea tukio la udhalilishaji ni kukaa na kumaliza nyumbani, hawaangalii madhara yanayompata mwathirika. Nakuombeni tuache tabia hizi kwani kufanya hivyo tunawaweka watoto wetu katika hatari zaidi ya kufanyiwa udhalilishaji,” alisema.
Mkuu wa upelelezi na mratibu wa dawati la kijinsia kutoka jeshi la polisi Wete, Fakih Yusuf Mohammed, aliitaka ijamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale linapotokea tukio la udhalilishaji ili uchunguzi ufanyike na hatimae kila mmoja apate haki anayostahiki.
“Tunafahamu kuna baadhi ya akari polosi si waadirifu lakini nakuombeni ukimwona askari polisi anakushawishi upatane na mdhalilishaji ili kuimaliza kesi kataa. Sisi jeshi la polisi tunahitaji taarifa kutoka kwenu ili tufanye kazi yetu,” alisema.
Juma Musa Omar kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, alisema serikali kupitia ofisi hiyo imeweka mkakati wa kuzisimamia kesi za udhalilishaji ili kuhakikisha zinapata hukumu na washitakiwa wanatumikia adhabu kwa mjibu wa sheria pale wanapotiwa hatiani.
“Sisi tuna mkakati maalumu tunaokwenda nao. Sasa hatufuti kesi hata moja ya udhalilishaji kwa mtu anayekuja kutaka tuifute kesi hiyo, au anaegoma kuja mahakamani kutoa ushahidi, kwani tumegundua wengi wanatumia mwanya huo wa kutokwenda kutoa ushahidi ili muda ukifika kesi yao ifutwe,” alisema.
Awali Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said, alisema mkutano huo ni mwendelezo wa juhudi za TAMWA Zanzibar kuisaidia serikali kupambana na vitendo vya udhalilishaji katika jamii kwa kutoa elimu ya ufuatiliaji na utoaji wa ushahidi mahakamani ili kujenga jamii inayozingatia usawa na usalama wa kila mmoja.
Alisema wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa vitendo vya udhalilishaji, hivyo kuna haja kwa jamii kushirikiana ili kudhibiti vitendo hivyo.