NA MWANDISHI WETU
ALIYEKUWA Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, bado ataendelea kuwa ni kielelezo cha ushujaa kwa Wazanzibari kutokana na matendo yake yaliobaki kuwa tafsiri halisi ya uzalendo na maendeleo.
Kiongozi huyo licha ya kuwa shujaa na mwana Afrika halisi, alipigania maslahi ya wananchi wanyonge na masikini, bila kuchoka hadi pale uhuru kamili wa Zanzibar ulipopatikana Januari 12, mwaka 1964.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mzee Ali Ameir Mohamed, akiwa kijijini kwake huko Donge Kichavyani kisiwani Unguja katika mahojiano maalum ya kumbukumbu ya miaka 49 tokea kuawa kwa Rais huyo wa kwanza April 7, mwaa 1972.
Mzee Ameir, alisema viongozi wengi katika bara la Afrika wamekuwa na tabia ya kutoa misimamo mingi inayohusu utetezi wa maslahi ya watu wote wanapokuwa nje ya madaraka, na pale wanapokalia viti vya utawala hujisahau na kutenda kinyume na ahadi zao.
Alisema ahadi za chama cha ASP kupitia Manifesto yake ya kwanza ya uchaguzi toka mwaka 1957, na ahadi za Rais Mzee Karume ilisimamiwa ipasavyo katika utekelezaji ulioleta manufaa chanya yenye tija kwa wananchi na maendeleo ya nchi yao.
“Nathubutu kusema kinagaubaga Hayati sheikh Abeid Amani Karume ameuawa akiwa kielelezo cha ushujaa kutokana matendo yake mema .Utekelezaji wa ahadi zake kwani dhana ya uzalendo na maendeleo amezitekeleza na aliyaahidi ametenda na alioyaacha yamebaki kuwa alama ya maendeleo” Alisema Mzee Ameir.
Waziri huyo wa zamani akimzumgumzia hayati Mzee Karume ,amelitaja jina lake halitachakaa na kusahaulika kwa kuwa alijitolea maisha yake yote kuhakikisha Zanzibar inafika mbali kimaendeleo katika kujenga ustawi wa maisha ya watu chini ya umoja, amani alipinga ubaguzi ,ukabila na udini.
Aidha, Mzee Ameir amesema, kabla ya kuingia madarakani chama chake ASP kuliweka msimamo wake bayana na kusema kikifanikiwa kushika madaraka kitavunja matabaka ya ubwana na utwana ,kukomesha ubaguzi na kuhimiza watu kushirikiana na kufanyakazi za kimaendeleo.
“Mzee wetu Karume aliamini katika msimamo uliowataka wananchi kufanyakazi kwa bidii,huthaminiwa kwa utu na heshima ya kila mmoja .Hakutaka uzembe, uvivu na porojo .Hakusita wala kuogopa kusema kweli hivyo amekufa akiwa shujaa wa kweli na mzalendo kwa Zanzibar na Afrika “Alisksitiza
Mwanasias huyo, aliyewahi pia kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Habari, alisisitiza na kutaka kizazi kipya kuisoma historia ya nchi yao mahali ilipotoka, ilifikaje mahali walipo na kuona jinsi watakavyoilinda nchi yao bila kupotoshwa.