NA MWANDISHI WETU

WAKATI leo Aprili 7, 2021 Zanzibar na Tanzania kwa jumla zinaadhimisha kumbukumbu ya kifo cha marehemu mzee Abeid Amani Karume, ni vyema tuhakikishe kumuenzi kwetu kunaakisi mambo mazuri aliyoyaazimia wakati wa uhai wake.

Ni dhahiri kuwa utamaduni wa kuwaenzi viongozi wa aina ya mzee Karume walioifanyia makubwa nchi yetu ni mzuri na unaofaa kuendelezwa.

Lakini tunapoandaa mambo mbalimbali kwa ajili ya kumbukumbu hiyo, tunapaswa tuuone umuhimu wa kutekeleza yale yenye manufaa aliyoyakusudia kuitendea nchi kwa faida ya wananchi wote.

Kila aliyemfahamu kiongozi huyo wa kwanza na mwanamapinduzi wa Zanzibar, bila shaka anaelewa dhamira aliyokuwa nayo ambapo baadhi ya mambo aliyaanza mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Mambo hayo ya maendeleo yapo mengi na hakuna haja ya kutaja hapa orodha yote, lakini kubwa ambalo mzee wetu alilisimamia kikamilifu, ni kupinga dhuluma dhidi ya wananchi.

Kwa moyo mweupe, marehemu mzee Abeid Amani Karume alitaka wananchi wote watendewe haki na asitokee mtu wa kuwadhulumu au kuinua mkono kuwadhuru kwa namna yoyote.

Na kwa hivyo, vitendo vya kuwapiga danadana wananchi pale walipofika katika ofisi za serikali kufuata huduma, havikuwa na nafasi hata chembe.

Kila kiongozi na mtendaji alijua wajibu wake na dhima aliyokubali kuibeba, na pia nidhamu kazini ilikuwa kipaumbele namba moja katika uwajibikaji.

Kila mfanyakazi aliyepewa dhamana ya kuwahudumia wananchi alihakikisha urasimu hautamalaki kuharibu sifa za Wizara, Idara, Shirika au taasisi yoyote ya umma aliyokuwa akitumikia.

Tangu mzee Karume alipopoteza maisha kwa kuuawa tarehe 7 Aprili, 1972, tumekuwa tukiendeleza utaratibu wa kumkumbuka kwa mambo mbalimbali ikiwemo makongamano katika vyuo na taasisi nyengine pamoja na kumuombea dua.

Lakini, ili maadhimisho hayo ya kifo chake yaweze kuwa yakinifu, haitoshi tu kufanya mambo niliyoyataja hapo juu, bila kuhakikisha sote, kuanzia viongozi mpaka watendaji wa sekta ya umma, binafsi na wananchi, tunafuata kikamilifu nyayo zake kwa kuendeleza mema aliyowahi kuyafanya na aliyokuwa ameyapanga.

Kiongozi wetu huyo mpendwa alikemea ubaguzi wa aina yoyote katika suala la kutoa haki kwa wenye kustahiki, pamoja na kupiga vita rushwa kwa vitendo akisema kuwa haki hainunuliwi.

Hata hivyo, katika miaka hii, kunashuhudiwa mmong’onyoko mkubwa wa maadili kwenye utumishi wa umma ambapo mambo yanayokwenda kinyume na dhamira ya muasisi huyo wa Mapinduzi yamekuwa yakifanywa dhahiri shahiri.

Baadhi ya watendaji kwenye mamlaka zinazotarajiwa kutoa haki kwa wananchi, wamekuwa wa kwanza kutenda kinyume na miongozo ya dhamana zao hali inayoibua manung’uniko mengi hasa pale wananchi wanapolazimishwa kuvaa ‘shati za mikono mirefu’ kununua haki.

Tunafahamu kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi mahiri na adilifu wa Dk. Hussein Ali Mwinyi, inachukia dhuluma kwa wananchi na ndio amevipa meno vyombo mbalimbali vya kusimamia haki ikiwemo Mamlaka ya Kudhibiti Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA).

Pamoja na kuchukizwa huko kwa serikali na jitihada inazochukua kukomesha vitendo vibaya vinavyopingana na dhamira ya mzee Karume, bado wapo watendaji wanaoendeleza vitendo hivyo.

Hawa wanapokuwa mbele ya watu hujionesha kuwa ni wasafi, lakini kumbe ni fisi waliovaa ngozi ya kondoo kwani wamekuwa wakiendeleza dhuluma kwa wananchi na hujuma za kiuchumi.

Kwa kuhitimisha waraka huu, nitoe wito kwa kila mwananchi wa Zanzibar, awe kiongozi wa ngazi yoyote au raia wa kawaida, kuhakikisha imani zao kwa kiongozi huyu tunayeadhimisha kifo chake kinachotimia miaka 49 leo, zinakwenda sambamba na kufuata mema yote aliyofanya na aliyonuia kabla ya kufumba jicho.

Mwenyezi Mungu amuweke pahala pema Peponi mpendwa wetu, marehemu Abeid Amani Karume. AMIN.