NA MWANDISHI WETU

THAMANI ya biashara kwa mwezi Februari 2021, umeonyesha nakisi ya shilingi bilioni 86.8, nakisi ambayo imeongezeka kwa asilimia 37.8 ukilinganisha na mwezi Januari.

Hayo yamebainishwa wakati wa uwasilishaji wa takwimu za biashara za kimataifa kwa mwezi Februari huko Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mazizini mjini Unguja jana.

Mkuu wa Kitengo cha Utoaji wa Huduma, Bakar Khamis Kondo, alisema, ikilinganishwa na mwezi Februari 2020, nakisi hiyo imeongezeka kwa asilimia 47.8.

Alisema, bidhaa zilizosafirishwa  zilifikia shilingi milioni 4,176.4 huku zikipungua  kwa asilimia 74.5% ukilinganisha na mwezi Februari 2020 na imeongezeka kwa aslimia 100 ukilinganisha na mwezi Januari 2021.

Alisema, asilimia 57.6% ya thamani yote  ya usafirishaji kwa ilichangiwa  na usafirishaji wa vyakula na wanyama hai na kuzitaja bidhaa zilizosafirishwa kuwa ni pamoja na mwani, pumba na wanyama hai.

Alisema, Denmark iliongoza kwa bidhaa zilizokuwa na thamani ya shilingi milioni 2,717.1 sawa na asilimia 65.1, ikifuatiwa na Vietnam, Marekani, China na India.

Akizungumzia takwimu za uagizaji wa bidhaa, alisema, ziliingizwa bidhaa za thamani ya shilingi  milioni 90,982.5, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.2 ukilinganisha na mwezi Februari 2020 na asilimia 41.9 ikilinganishwa na mwezi Januari 2021.

“Kundi la mashine na vifaa vya usafirishaji limechangia  asilimia 36.9 ya bidhaa zote zilizoagizwa nchini katika jumla hiyo”, alifafanua Kondo.

Mchumi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Ulrick Mumburi, alisema, ipo haja ya kuongezewa thamani kwa bidhaa zinazosafirishwa nje ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni.