Licha ya changamoto watimiza miaka 57

NA MWANDISHI WETU

WAKATI muungano wa nchi mbili za ukanda wa Afrika Mashariki, Zanzibar na Tanganyika uliozaa taifa la Tanzania leo ukitimiza miaka 57, ni jambo la kujivunia kwamba unabaki kuwa muungano wa kupigiwa mfano barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Ni ukweli ulio dhahiri kwamba muungano huo hauna mfano wake ikizingatiwa kuwa ziko nchi nyengine nyingi zilizowahi kuungana lakini kwa sababu mbalimbali zilishindwa njiani.

Ikumbukwe kuwa, chini ya waasisi wa taifa hilo, hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanganyika huru na marehemu Abeid Amani Karume Rais wa kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, nchi hizo zilikuja kuungana baada ya mashauriano ya viongozi hao na wasaidizi wao wakiwawakilisha wananchi wa pande mbili.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa, baada ya Tanganyika kupata uhuru wake Disemba 9, mwaka 1961, haikuchukua siku nyingi nchi hiyo kupata kiti katika Umoja wa Mataifa mnamo tarehe 14 Disemba mwaka huohuo.

Kiti cha Tanganyika katika Umoja wa Mataifa ilikuwa ‘GA Resolution 1667 (XVI)’. Aidha kupitia uhuru wake wa tarehe 9 Disemba, 1963, Zanzibar ilipata kiti cha Umoja wa Mataifa mnamo tarehe 16 Disemba, 1963 namba yake ikiwa ‘GA Resolution 1975 (XIII)’.

Hata hivyo, mnamo Novemba 2, 1964, Zanzibar na Tanganyika zilipoungana na kuunda Tanzania, iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje iliuandikia Umoja wa Mataifa kutaka nchi hizo (Zanzibar na Tanganyika) ziondoshwe na taifa lao moja lijulikane kwa jina la Tanzania.

Ipo mifano kadhaa ya nchi zilizowahi kuungana ambazo hazikuweza kudumisha miungano yao kama ilivyo kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mfano muungano wa Syria na Misri uliofanyika mwaka 1958, ulidumu kwa miaka mitatu tu na mwaka 1961 Syria iliamua kujitoa baada ya kutoridhika kutokana na uendeshaji wa baadhi ya mambo.

Jengine ni Shirikisho la ‘Senegambia’ ambalo lilikuwa baina ya Senegal na Gambia, nchi zilizoko Afrika Magharibi lililoundwa mwaka 1981 na lilikuja kufa mwaka 1989 baada ya kudumu kwa miaka saba tu, Gambia ikikataa kuendelea na muungano huo kwa sababu kadhaa.

Lakini muungano mwengine ni ule wa Kisovieti (Urusi), baina ya Russia na jamhuri nyengine za Kisovieti ambao ulisambaratika mwaka 1999 baada ya kuwepo kwa takriban miaka 80.

Mfano mwengine ni nchi ya Eritrea iliyokataa kubakia ndani ya Ethiopia na kuamua kushika bunduki kupigana na majeshi ya Ethiopia wakitaka kujitenga baada ya zaidi ya miaka 20 ya kuwa chini moja.

Kwa upande mwengine, nchi ndogo ya Timor Mashariki huko Kusini Mashariki ya bara la Asia, baada ya ukoloni wa Wareno kuondoka nchini mwao mwaka 1975, hawakukubali nafasi yao ichukuliwe na nchi kubwa jirani, Indonesia na walipigana hadi walipojikwamua mwaka 2002.

Lakini kwa nchi za Afrika Magharibi, Muungano wa kwanza ulikuwa kati ya Ghana na Guinea mwishoni mwa miaka 50 na mwanzoni mwa miaka 60, ambapo baadae Mali ikajiunga nao.

Muungano huo ulitokana na vuguvugu la umajimui wa Afrika (Pan Africanism), vinara wake wakiwa Kwame Nkrumah wa Ghana, Sekou Toure wa Guinea na Modibo Keita wa Mali.

Katika muktadha huo, Novemba 1958 uliundwa muungano wa Ghana na Guinea mara baada ya mkutano wa Waafrika (All African Peoples Conference).

Ghana ilitoa fedha nyingi na kuipa Guinea ili ijitoe haraka kutoka katika utegemezi wa Ufaransa na Mei 1959, ikatangazwa kuwa umoja huo utatambulika kama ‘Umoja wa Dola za Kiafrika.’

Ilipofika Aprili 1961, Mali nayo ilijiunga na umoja huo ambao hata hivyo ulivunjika mwaka 1962 kutokana na vita baridi, ambapo Guinea ilionekana ikinyooshea mikono Marekani wakati wenzake walikuwa wakifuata mrengo wa kushoto wa Karl Marx/Lenin.

Kudumu kwa muungano wa Tanznaia kwa zaidi ya nusu karne sasa, kunaonesha wazi umuhimu wake kwa Watanzania, na kwamba changamoto zinazojitokeza mara kadhaa ni mambo yanayoweza kuwekwa sawa kwa viongozi/tume za pande hizo kukaa pamoja kama inavyofanyika kila baada ya muda.

Bila shaka Muungano ni zoezi endelevu na kila inapohitajika kuufanyia marekebisho au mabadiliko yenye lengo la kuuimarisha zaidi ni kwa manufaa ya wananchi vyema kufanya hivyo.

Kwa vyovyote vile, muungano huu kutimiza umri wa miaka 57 ni jambo la fahari kwa Watanzania licha ya vigingi vyote wanavyokutana navyo njiani, ambavyo kutokana na busara za viongozi wamekuwa wakivuka na safari kuendelea kwa salama na amani.

Watanzania wana haki ya kutembea vifua mbele kwa sababu wamezipiku nchi nyingi zilizojaribu kuungana lakini zikashindwa njiani.

Kuonesha uimara na ukomavu wa Muungano wa Tanzania, jaribio la baadhi ya wananchi kumi kutoka Zanzibar kwenda kuulalamikia mahakamani wakidai waoneshwe mkataba halisi wa tarehe 26 Aprili, 1964 liligonga mwamba.

Utata juu ya suala hilo ulimalizwa ikulu jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 14 Aprili, 2014, pale mkataba wa muungano ulipoletwa hadharani mbele ya waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari, na wananchi kuona kupitia televisheni.

Baada ya Bunge maalumu la katiba kuomba hati hiyo halisi, ilipelekwa bungeni humo tarehe 16 Aprili, 2014 na kila mbunge akapatiwa nakala.

Ili muungano uzidi kuwa imara na wenye maslahi kwa wananchi wa pande zote, ni lazima kuwe na nia njema kwa viongozi kwenda kwa wananchi, na asitokee mtu kukubali au kupinga kitu kwa kuangalia utashi na maslahi yake binafsi.

Tume inayoshughulikia kero za muungano lazima zisafiane nia na zisisukumwe na ‘U-SISI NA U-WAO’. Katika suala hilo la dhamira njema, tume hiyo yenye uwiano sawa wa pande zote mbili za muungano, kwa kazi nzuri na adilifu inaoifanya chini ya Mwenyekiti wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Katika jumuiya au mikusanyiko ya watu mbalimbali, hakukosi kutokea hitilafu, lakini zisitumike kuwagawa bali ziwaongezee nguvu ya kushikamana kwa upendo huku wakishirikiana kuondosha tafauti zao.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una faida kwa pande zote mbili, ambapo wananchi wote ni wamoja, ndugu na kila mtu ana haki na uhuru wa kuishi sehemu yoyote ya Tanzania na kufanya shughuli halali kujiendeshea maisha ili mradi havunji sheria.