NA HASHIM KASSIM
KOCHA mkuu wa timu ya wanawake ya Green Queen FC Salim Kibed amesema kuna ugumu mkubwa wa kuwapata wachezaji wa mpira wanawake hapa visiwani Zanzibar.
Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na gazeti hili katika uwanja wa Ziko Kiembe samaki kwenye mazoezi ya timu hiyo.
Kibedi alieleza kuwa kitendo cha kutokuwepo wachezaji wa kutosha kinachangia kusuasua hata kwa ligi soka ya wanawake hapa Zanzibar.
“Kupatikana wachezaji wanawake hapa Zanzibar ni ngumu ndio maana unaona hata kwenye mazoezi wanafika kwa idadi ndogo jambo ambalo linainyima uhai ligi ya wanawake” alisema.
Alisema kukosekana wachezaji wa kutosha sio kwenye timu ya Green Queen FC pekee bali ni tatizo linaloikumba Zanzibar nzima hasa timu za uraiani, na hii ndio sababu ya kutokuwa na kiwango kizuri katika mashindano.