NA JOSEPH DAVID
BEKI kisiki wa kimataifa anayekipiga kwenye timu ya Simba na timu ya taifa ya Kenya Joash Onyango, amesema wapo mguu sawa kukabiliana na wenyeji wao Al Ahly ya Misri kwenye mchezo wao wa mwisho katika hatua ya makundi.
Nyota huyo ambaye ameibuka na tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Machi kwa mashabiki ameyasema hayo kabla ya kusafiri na timu yake kuelekea Cairo Misri.
Alibainisha kuwa wachezaji wapo tayari kwenda kupambana kwa nguvu zote ili washinde mchezo huyo, licha ya kuwa tayari wamejihakikishia kuingia hatua ya robo fainali kwenye mashindano hayo ya ngazi ya juu kabisa kwa klabu barani Africa.
Onyango alisema anafurahia kushiriki michuano hiyo kwani anapata kukutana na wachezaji wakubwa kutoka mataifa tofauti barani Afrika, kitendo ambacho kinazidi kumuongezea changamoto katika kazi yake ya kusakata kabumbu.
Timu ya Simba ipo Cairo, nchini Misri kucheza mechi ya kukamilisha hatua ya makundi itakayochezwa siku leo kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika ya Mashariki.