Awataka wasitumie madaraka kama fimbo

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amewataka watumishi wa serikali kutotumia nyadhifa na madaraka waliyopewa kama fimbo ya kuwaadhibu watumishi walio chini yao.

Masoud alisema hayo jana katika semina ya mafunzo elekezi kwa makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu na viongozi wengine waandamizi serikalini wakati alipowasilisha mada katika semina hiyo.

Alisema nafasi walizokabidhiwa ni dhamana, hivyo hawapaswi kuzitumia kama fimbo kuwaadhibu, kuwatesa na kuwanyanyasa wafanyakazi walio chini yao.

“Tukiwekana kazini kwa sababu ya udugu, urafiki au itikadi za vyama vyetu basi ni wazi hatutofanikiwa kufanikisha malengo ya serikali.”  Suala hili ni moja ya changamoto kubwa inazozikabili sekta za umma visiwani Zanzibar.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanayolenga kuwaongezea ujuzi na maarifa watendaji wakuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yanafanyika katika hoteli ya Sea Cliff iliyopo Michungwa miwili wilaya ya Kaskazini ‘B’ mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika mada yake aliyoipa jina la ‘mambo ya msingi kwa utumishi wa umma’, Othman alisema tatizo kubwa lililopo ni baadhi ya watumishi wa umma kutokujali wajibu wao, jambo ambalo linasababisha kuzorotesha au kufelisha kabisa shughuli za serikali.

Aliongeza kuwa si vyema kwa viongozi katika taasisi kujiona hakuna zaidi yao na kuwadharau wengine, kwani jambo hilo huzusha chuki na kupunguza ufanisi kwa watendaji wa chini.

“Kuwa katika wadhifa mkubwa sio kibali cha kuwanyanyasa walio chini yako, kama mtendaji kakosea aadhibiwe kwa mujibu wa sheria na siyo kwa kumuonea”, alisema Makamu huyo.

Alisema wapo viongozi wakiondoka katika madaraka watendaji na wananchi wanafurahi sana wengine hata kufikia kufanya sherehe, hivyo aliwataka wakuu hao wasifikie mazingira ya kufanyiwa sherehe bali waweke mazingira rafiki na wafanyakazi wote.

Aidha aliwasisitiza viongozi hao kutilia maanani suala la kuhifadhi kumbukumbu. “Tujitahidi sana kuhakikisha katika wizara zetu taarifa za umma tunazihifadhi katika ofisi za nyaraka au gazeti la serikali ili kuweza kusaidia katika kumbukumbu zetu na kwa matumizi ya baadae”, alisema.

Makamu huyo alisema uzuri wa katiba na sheria hautasaidia ikiwa watumishi hawajaamua kubadili mitazamo kutoka walipo na kuelekea katika ngazi ya uwajibikaji itakayoleta ufanisi.