NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

ASKARI Polisi saba wakiwemo watano wa kituo cha Polisi Usa River wilayani Arumeru katika Mkoa wa Arusha na wawili wa kituo kikuu cha Polisi jijini Arusha wanashikiliwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Takukuru Mkoani humo kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni 100.

Imeelezwa kuwa Polisi hao na wananchi watatu wakazi wa Usariver wilayani humo, walimlazimisha mfanyabiashara, Profesa Justine Maeda Mkazi wa Lenganga ,Usariver awape rushwa ya kiasi hicho cha fedha wakidai anajihusisha na biashara ya meno ya tembo.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, James Ruge amethibitisha kushikiliwa kwa Watuhumiwa hao kwenye kituo kikuu cha Polisi Mkoani hapa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alisema hana taarifa rasmi kuhusu tukio hilo, ambalo Askari wake wanashikiliwa kwa Rushwa.

Inadaiwa kuwa, Polisi waliokamatwa ambao majina yao yanahifadhiwa ni pamoja wakaguzi wasaidizi wawili, Askari Koplo mmoja na Askari Kostebo wanne wakiwemo wawili wa kituo kikuu cha Polisi Arusha, waliodaiwa kutoroka lindo wakiwa na silaha wakaenda kufanya uhalifu katika Mji wa Usariver.

Chanzo cha habari hizi kinadai kuwa, wakati wa tukio la kukamatwa Polisi mmoja alitoroka na ushahidi wa meno ya tembo akiwa mikononi mwa Polisi.

Inadaiwa kuwa, mmoja wa raia watatu waliokamatwa (jina tunalihifadhi) aliwahi kuwa mfanyakazi wa shambani wa mfanyabiashara huyo wa Mji wa Usariver na alifukuzwa kazi muda mrefu uliopita.

Chanzo cha habari hizi kinadai kuwa raia huyo ndiye aliyeshawishi Polisi wadai rushwa kwa bosi wake wa zamani kwa madai kwamba mfanyabiashara huyo ni muoga wa Polisi.

Ilidaiwa kuwa, mtuhumiwa huyo aliwaeleza Polisi watafute meno ya tembo wayaweke kwenye moja ya mizinga ya nyuki shambani kwa mafanyabiashara huyo, ili wamtuhumu kuwa anafanya biashara haramu na kwa kuwa ni muoga atakubali kutoa rushwa ya kiasi chochote cha pesa.

Inadaiwa kuwa Polisi wanaotuhumiwa kutoka kituo cha Polisi Usariver kwa kushirikiana na raia hao walitekeleza mpango huo na siku ya upekuzi Polisi wawili wenye silaha kutoka Arusha mjini walikwenda kwenye eneo la tukio, ili kumuaminisha mfanyabiashara huyo kuwa upekuzi ni halali na na viongozi wa polisi Usa na Kituo Kikuu Arusha wanajua kitu ambacho sio kweli.

Taarifa zinadai kuwa shamba la mfanyabishara huyo lina mizinga mingi ya nyuki lakini katika upekuzi huo Polisi walikwenda moja kwa moja katika mzinga walikoficha meno ya tembo, na kumuonesha mfanyabiashara huyo kuwa anafanya biashara haramu hivyo anastahili kushitakiwa kwa uhujumu uchumi.

 

Inadaiwa kuwa mfanyabiashara huyo aliwapa shilingi milioni 67 alizokwenda kuchukua katika benki ya NMB na CRDB zilizoko katika Mji wa Usariver na kiasi kingine cha fedha cha shilingi milioni 33 aliomba kwa ndugu na kukamilisha kiasi cha shilingi milioni 100 walizoomba askari hao.