NA MWANDISHI WETU

NYOTA ya mfanyabiashara na bilionea kijana barani Afrika, Mohamed Dewji anayemiliki kampuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL) inazidi kung’ara baada ya rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa kumteua kuwa mshauri wake katika masuala ya kiuchumi.


Uteuzi huo utakaodumu kwa miaka mitano unaonyesha namna rais Ramaphosa anavyothamini mchango wa uwekezaji ambao Mo Dewji kaufanya na kuchochea ukuaji wa uchumi katika nchi mbalimbali barani Afrika ambako kampuni zake zimewekeza na kutoa ajira nyingi.


Rais Ramaphosa amemteua Mo Dewji kuwa mjumbe kwenye Baraza la Ushauri la Rais kuhusu uwekezaji ambalo lina jukumu la kuhakikisha nchi hiyo inapiga hatua kiuchumi kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi hiyo.


Kiongozi huyo wa Afrika Kusini alisema ana imani Dewji atawaongezea nguvu kwenye mikakati yao ya kuitangaza nchi hiyo kwenye sekta mbalimbali zitakazosaidia kuvutia wawekezaji na hatimaye kukuza uchumi wa taifa hilo ambalo ni miongoni mwa mataifa yaliyopiga hatua kubwa kiuchumi barani Afrika.


Kwa mujibu wa barua ya uteuzi wa Mo Dewji, Rais Ramaphosa alisema Baraza hilo lina jukumu la kumshauri Rais na Serikali ya Afrika Kusini juu ya kuvutia wawekezaji, kukuza na kuboresha mazingira ya uwekezaji wa ndani na nje ya nchi hiyo.


Baraza hilo la ushauri litakuwa jukwaa la kuchakata mawazo, kubaini vikwazo na kutafuta njia bora za kukuza ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi, wadau wa maendeleo na mawakala wa uwekezaji ili Afrika Kusini iongeze kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia.


Kutokana na uteuzi huo Mo Dewji atapata fursa ya kuhudhuria vikao mbalimbali vitakavyoandaliwa ndani na nje ya Afrika Kusini ambavyo vitawahusisha wafanyabiashara, viongozi wa serikali, vinavyolenga ukuzaji wa uchumi na kuwavutia wawekezaji.


Fursa hiyo itamuwezesha kutoa uzoefu wake juu ya uwekezaji, changamoto na utatuzi ili kuwezesha uchumi wa Afrika Kusini kukua zaidi.

Akizungumzia kuhusu uteuzi huo, Mo Dewji alisema anafurahi kwa kuwa inaonyesha viongozi wa Afrika wanavyotambua na kuthamini mchango wa wawekezaji wa ndani.

“Ni heshima kubwa kwangu ninaahidi kutumia uzoefu na maarifa yangu kufanikisha malengo yaliyokusudiwa, naamini tukishirikiana tutapiga kasi kwenye maendeleo” alisema Mo


Dewji amejizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya bara la Afrika kutokana na uwekezaji wake alioufanya kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda, usafirishaji na kwenye michezo ambapo ni mwekezaji katika timu ya Simba inayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara na hivi sasa inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa katika hatua ya robo fainali.


Hivi karibuni jarida la Forbes lilimtangaza Dewji kuwa bilionea kijana aliyeshika namba 13, mfanyabiashara huyo alisema analenga kukuza wigo wa ajira nchini Tanzania kwa kutoa ajira 100,000.