NA LAYLAT KHALFAN
MFANYABIASHARA maarufu hapa nchini, Mohamed Raza, amewataka wafanyabiashara wenzake kujaribu kuwasaidia wananchi wao kwa kuwarahisishia ujikimu futari katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mfanya biashara huyo ambae pia ni Mwanasiasa Mkongwe, aliyasema hayo wakati alipokutana na vyombo vya habari kwa lengo la kutoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya sita,inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambae anaiongoza bila ya kuyumba.
Alisema wafanyabiasha wakubwa wana nafasi ya kutumia zakka kwa kusaidia chakula wananchi wanyonge, ili kukidhi mahitaji yao na si vyema kuona baadhi ya wananchi wanakula mlo mmoja kwa siku, hivyo ni lazima wawe na huruma katika kuwasaidia hususan katika mwezi huu wa mfungo.
Akizungumzia suala la ushuru, Raza alisema isiwe kisingizio cha kuwakandamiza wananchi.
“Lazima tuishi tukiwa tunamuogopa Mungu tusikubali kutumiwa na watu wachache kwa kuzitia sumu serikali zetu”, alisema Mfanyabiashara huyo.
Akizungumzia kuhusu kodi, aliwataka wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kulipa kodi ili nchi iweze kuwa na maendeleo.