NA MADINA ISSA         

MKUU wa mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amekemea tabia ya baadhi ya wafugaji katika kijiji cha Charawe kuzuia mifugo yao kuzurura katika maeneo ya skuli na sehemu za kilimo.

Aliyasema hayo huko Charawe wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni muendelezo wa utaratibu aliojipangia wa kupita kwenye shehia kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Alisema kuiachilia mifugo kuzurura kunasababisha hasara kwa wakulima kwani wanaharibu mazao na kuzurura ovyo ni kusababisha uharibifu wa mazingira.

Hivyo aliwataka wananchi kudhibiti mifugo yao na iwapo kama watashindwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Aidha, mkuu huyo, aliliagiza baraza la Mji wilaya ya Kati kumchukulia hatua za kisheria mfugaji yoyote atakaekamatwa mifugo yake.

Nao wananchi wa kijiji hicho, waliomba serikali mkoani humo kuwapatia vifaa vya uokozi (life jacket) kwa walimu wanaotoka Chwaka kwenda kijiji hicho kwa usalama wa maisha yao.

Akizungumzia suala la wizi wa mazao na majumbani mkuu wa wilaya ya kati Marina Joel Thomas, aliwataka wananchi hao kuunda vikundi shirikishi ili kuweza kuondokana na tatizo hilo.