NA MWANDISHI WETU, MWANZA

MKUU wa  Mkoa wa Mwanza John Mongela leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa michezo ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Uzinduzi huo utatanguliwa na maandamano ya wachezaji zaidi ya 700 wanaoshiriki kwenye michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, baiskeli, riadha, karata, bao na draft.

 Katika michezo ya netiboli iliyofanyika jana timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani imeiadhibu bila huruma Wizara ya Mambo ya Nje kwa kuwafunga mabao 80-4, hadi mapumziko washindi walikuwa mbele kwa mabao 41-2, yaliyofungwa na Mwanaisha Ally mabao  61 na Mery Mangi mabao  19, mabao ya Mambo ya Nje yalifungwa na Juneck Mbisse.

Katika mchezo mwingine timu ya Ikulu iliwafunga Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) mabao 40-8, wafungaji Anna Msulwa alifunga mabao 31, Sophia Komba mabao  manne na Irene Kanije mabao  matano,mabao ya TPDC yalifungwa na Elizabeth Luanda mabao  sita na Rehema Said mabao mawili.

Timu ya Tanesco iliwafunga wenyeji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa mabao 48-0, mabao ya washindi yaliyofungwa na Celestine Mbassa 45 na Agnes Ryoba matatu.

Katika mchezo wa soka timu ya Ukaguzi iliwafunga MWAUWASA, mabao 2-1, yaliyofungwa na Nyanda Mabuga na Cassian Luoga na bao pekee la MWAUWASA lilifungwa na Telesifori Mwajemu.

Mchezo mwingine uliokuwa mkali timu ya Wizara ya Kilimo iliwafunga Mambo ya Nje mabao 4-3, yaliyofungwa na Johnson Tamba mabao matatu na Ahmed Kinyunyu bao moja, huku ya Mambo ya Nje yalifungwa na Habibu Soud, Elly Chuma na Mikidadi Magole.

Katika michezo ya kuvuta kamba wanaume timu ya Wizara ya Mambo ya Nje waliwavuta Wizara ya Kilimo kwa mivuto 2-0, huku Tanesco wakiwashinda TPDC kwa mivuto 2-0, wakati Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wakiwashinda MWAUWASA kwa mivuto 2-0, nayo timu ya Uchukuzi ilipata ushindi wa chee wa mivuto 2-0 baada Ulinzi kushindwa kuonekana uwanjani.

Kwa mechi za wanawake timu ya Uchukuzi iliwavuta Tanesco 2-0, nayo TPDC iliwavuta MWAUWASA kwa 2-0.