NA KHAMISUU ABDALLAH
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar, inatambua mchango wa mashirika ya kimataifa katika kuimarisha usafi na mazingira kwa wananchi.
Hemed alisema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera na Uratibu wa shughuli za Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed katika uzinduzi wa ripoti ya tathmini ya upatikanaji wa huduma za maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira (SWASH).
Alisema katika kulitambua hilo serikali inakwenda sambamba katika utekelezaji wa viashiria vya maendeleo endelevu (SDGs) hasa mambo yaliyoainishwa katika lengo nambari sita linalohusiana na upatikanaji wa huduma ya maji, usafi wa mazingira kwa wote na lengo namba nne linalohusu upatikanaji wa elimu bora.
Alisema serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto katika kuimarisha mazingira bora ya kujifunza.
Aidha alisema shirika hilo limefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa malengo ya kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi na zinazoendana na wakati zinazohusiana na maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira katika skuli za serikali na binafsi zinapatikana.
Hata hivyo, alisema mpango huo wa maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira katika skuli unalenga katika kuhakikisha vyanzo vya maji safi na salama vinakuwepo katika skuli zote na yanapatikana katika vyanzo salama.
Hata hivyo alisema serikali inaendelea kutekeleza ilani ya CCM 2020/2025 inayosisitiza suala la ubora wa miundombinu ya kielimu ikiwemo suala la wanafunzi wanapokuwa katika maeneo ya skuli.
Alisema lengo hilo linakwenda sambamba na dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050 inayohamasisha mazingira bora ya miundombinu ya kujifunza kwa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Aliwapongeza wadau mbalimbali wa taasisi za kimataifa na jumuiya zisizo za serikali kwa juhudi kubwa za kuhakikisha upatikanaji wa mazingira rafiki ya kufundisha na kujifunza katika skuli ambayo inaongeza kazi ya maendeleo endelezu kwa nchi.
Kwa upande wake waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said, alisema suala la utunzaji wa miundombinu hasa ya vyoo ni muhimu sana hivyo aliziomba kamati za skuli kuhakikisha wanasimamia utunzaji wa mazingira ya ndani na nje ya skuli.
Akizungumzia ripoti hiyo alisema utafiti uliofanywa una manufaa makubwa kwa Zanzibar katika kuchochea maendeleo ya elimu.
Naye mwakilishi kutoka Shirika la kuhudumia watoto ulimwenguni (UNICEF), Frank Odhiambo alisema shirika hilo linasaidiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hasa katika miradi inayogusa sekta ya elimu.
Alibainisha kuwa Shirika lao litaendelea kusaidia hasa ujenzi wa sehemu ya kukosha mikono na vyoo kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya skuli za Zanzibar ili wanafunzi waweze kujikinga na maradhi mbalimbali hasa ya kipindupindu.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mayasa Mahfoud Mwinyi, alisema ripoti hiyo ni hatua muhimu ambayo itasaidia upatikanaji wa takwimu sahihi.
Alisema utafiti huo itasaidia sana wadau wengine hasa katika sekta ya elimu na kuamini kwamba matokeo hayo yatatumika katika kuandaa tafiti mbalimbali.