NA ZAINAB ATUPAE
TIMU ya Shangani inayoshiriki ligi daraja la pili wilaya ya Mjini Unguja leo inatarajia kucheza mechi ya kirafiki na Mafunzo inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar.
Akizungumza na gazeti hili huko uwanja wa Shangani Kikwajuni kocha mkuu wa timu hiyo Shangani Salim Riami,alisema mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa uwanja wa Miembeni majira ya saa 10:00 jioni.
Alisema licha ya timu yao kupitwa kwa madaraja na wapinzani wao,lakini watahakikisha wanapambana na kushinda ili kuonesha heshima ya klabu yao.
Alisema timu ipo vizuri na juzi walicheza mechi ya kirafiki na Kundemba inayoshiriki ligi daraja la pili Mkoa na kutoka sare ya mabao 2-2.
“Kwa matokeo hayo ni dhahiri kuwa timu yetu sio ya masihara na tunamini mechi hiyo tutafanya vyema,”alisema.
Abdalla Bakar ‘kocha Edo’ kocha wa Mafunzo,alisema mechi hiyo kwao ni burudani na ushindi kwao ni lazima.
Aidha alisema katika kipindi hichi cha mapumziko walicheza mechi tatu za kifaki kwa ajili ya kujiandaa na muendelezo wa mechi za ligi.
Edo alisema anajindaa na mechi ya ligi kuu wanayotarajia kucheza na Chuoni siku ya Jumatano.