NA SALUM VUAI
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohammed Said, amezindua programu ya udhamini wa masomo kwa wanafunzi Wazanzibari katika skuli pekee ya kimataifa visiwani humu, ‘International School of Zanzibar’ iliyopo Mbweni.
Udhamini huo wa mwaka 2021 utakaochukua miaka minne utahusu watoto wa skuli hiyo wenye hali duni ya kipato, ambao utatolewa kwa mtoto mmoja kusoma kwa muda wa miaka minne ya elimu ya sekondari akilipiwa gharama zote na utakuwa endelevu.
Akizungumza na wazazi na uongozi wa skuli kabla kuzindua programu hiyo, Simai alisema serikali inafarijika kwa mchango mkubwa unaotolewa na wadau binafsi wa sekta ya elimu ambao unaunga mkono juhudi za kuinua elimu nchini.
Alisema serikali inafurahishwa kuwa pamoja na skuli hiyo kujumuisha wanafunzi wengi wa kigeni, lakini kutokana na mabadiliko ya kimaisha hata Watanzania wanaopenda kupeleka watoto wao wanapokelewa iwapo wanakidhi vigezo.
Aliupongeza uongozi wa skuli hiyo, kwa kuchanganya watoto wa mataifa mbalimbali wakiwemo Watanzania, akisema utaratibu huo unawawezesha wanafunzi kujifunza tamaduni tafauti.
Kwa upande mwengine, alitoa rai kwa uongozi wa skuli hiyo kuwafuatilia wanafunzi waliopitia hapo ambao wametawanyika na kuajiriwa katika mataifa mbalimbali, wamefanikiwa na wanafanya mambo makubwa.
Kuhusu programu hiyo, Simai alieleza kuwa, kitendo cha kuishirikisha serikali kwenye uzinduzi huo, ni ishara ya kuwepo ushirikiano mzuri kati yao, ambao ni muhimu katika kuimarisha elimu ya watoto wa Tanzania.
Hata hivyo, Simai aliwataka wazazi na walezi, kuchukua juhudi ili kuiunga mkono serikali katika kusimamia masomo ya watoto wao, akisema uwili huo ni muhimu kwani mtu hawezi kupiga kofi kwa mkono mmoja.
Mapema, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa skuli hiyo Yvonne Karume, alisema udhamini huo utatolewa kwa mwanafunzi wa kidato cha tatu ukihusisha ada ya masomo, sare za skuli, vitabu, kompyuta, ada za mitihani ya Cambridge, chakula na safari za masomo, ukigharimu shilingi 32,000,000 kwa mwaka.
Alisema mwanafunzi atakayechaguliwa, atajumuika katika shughuli zote za kiskuli, na kwamba udhamini huo utadumu muda wote wa masomo hadi atakapohitimu kidato cha sita, na kwamba kila mwaka (2021-2024) fursa nyengine itatolewa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, maombi ya udhamini yatapokelewa na kuchujwa na kamati maalum na baadae kufanyiwa tathmini ya kitaaluma kabla kupata mshindi.
Alivitaja vigezo vitakavyotumika kuwa ni, matokeo ya mtihani wa kidato cha pili (Alama ‘A’ kwa masomo ya Kiingereza na Hisabati) sambamba na kuandika insha ya maneno 500 kwa lugha ya Kiingereza.
‘International School of Zanzibar’ (ISZ), ni skuli pekee hapa Zanzibar iliyoidhinishwa kuwa ya kimataifa ikitoa huduma kwa wageni na wenyeji tangu mwaka 1988, ikifuata mitaala ya Cambridge (IGSA) pamoja na sekondari ya juu (A Level).