NA KHAMISUU ABDALLAH

TUME ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, imesema kukamilika kwa sheria ya huduma ndogo ndogo za kifedha (Microfinance) itasaidia kuweka usalama wa fedha za wananchi kupitia benki, vikundi vya kuweka na kukopa na SACCOS.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Khadija Shamte Mzee, aliyasema hayo wakati akifungua kikao kilichoshirikisha tasisi za umma zinazohusika na sheria ndogo ndogo za kifedha katika Ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini.

Aidha alisema sheria hiyo inalenga kuweka utaratibu mzuri wa fedha za wateja na zinakuwa salama kwa kuzisimamia ipasavyo.

Alisema kabla ya kuwepo sheria hiyo wananchi wamekuwa wakipata changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa fedha zao kutokana na kutokuwepo na sheria inayomlinda mteja.

Alisema hivi karibuni imeshuhudiwa baadhi ya wananchi kupoteza pesa kwenye kampuni ya Master Life pamoja na kutokuwepo kwenye utaratibu wa kifedha.

Mwenyekiti Khadija, alisema mara nyingi tasisi ya fedha inapojitokeza athari basi wanaoathirika zaidi ni wateja hasa wale wenye kipato cha chini waliowekeza fedha zao.

Hata hivyo alibainisha kuwa Zanzibar sasa itakuwa na sheria rasmi ambayo itasimamia masuala yote ya huduma ndogo ndogo za kifedha ili kuona kila mwananchi aliwekeza basi anapata haki yake.

“Sasa kutakuwa na sheria makini na itaweka utaratibu wa kusimamia kuona inapojitokeza changamoto pesa za wateja zinapatikana,” alisema.

Kwa upande wa SACCOS na vikoba vya kuweka na kukopa alisema sheria hiyo itawezesha na kusaidia kukua kimtaji na kuwasaidia wananchi kwa lengo walilokusudia kwani imebainika kuwa Zanzibar SACCOS nyingi zina uwezo mdogo wa kifedha.

Mwanasheria kutoka tume hiyo, Nassor Ameir Tajo, alisema tume hiyo ni chombo cha kiutafiti kwa sheria mbalimbali, ili kuhakikisha sheria zote hazileti mgongano kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

Alibainisha kuwa lengo la sheria hiyo ni kuondosha changamoto na malalamiko ya wananchi kuchukuliwa pesa zao na kukimbia kwa baadhi ya tasisi kutoka Tanzania bara kuja Zanzibar na kufanya biashara kwa kuchukua fedha za watu.

Alisema imebainika kuwa hayo yote yanajitokeza kutokana na kuwa na mwanya wa kutokuwepo kwa sheria hiyo.

“Sasa katika kuondoa mwanya huu ndipo serikali ilipoleta sheria hii haraka ili kuondoa tatizo la wananchi kudhulumiwa fedha zao hapa Zanzibar,” alisema.

Hivyo, alibainisha kwamba wananchi watarajie mafanikio makubwa kwa ujio wa sheria hiyo ikiwemo kuondosha dhulma na kuona serikali inafaidika kwa kuweza kudhibiti uendeshaji wa biashara za kifedha kwa wananchi wa kipato cha chini.

Mohammed Maulid Mohammed ambae ni Ofisa Ufatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, alisema mkutano huo una manufaa makubwa kuona wanapitia sheria hiyo ambayo itaweza kusimamia biashara ya utoaji wa huduma ndogo ndogo za kifedha kwa upande wa Zanzibar.

Alisema awali Zanzibar ilikuwa haina sheria hiyo lakini hivi sasa uwepo wake itaweza kusimamia tasisi zote zinazotoa huduma za kifedha ikiwemo mabenki, SACCOS na mashirika yanayotoa mikopo na wanaochukua fedha kutoka kwa wananchi.

Mbali na hayo, alibainisha kwamba sheria hiyo pia itasaidia wananchi kupata huduma zilizokuwa bora na kumlinda mteja wakati wote.

Nao wadau walioshiriki katika kikao hicho, walisema ujio wa sheria hiyo utasaidia kuwa na dhana ambayo itaweza kuwasaidia hasa wajasiriamali wadogo wadogo katika kupata huduma za kifedha.

Njuma Ali ni Katibu wa Melinne SACCOS, alisema sheria hiyo ina manufaa makubwa kwao hasa katika kuweka usalama wa fedha zao na kuondosha changamoto ya ulipaji wa kodi nyingi kwenye tasisi tofauti.

Mkutano huo wa siku moja uliwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo kutoka Benki kuu ya Tanzania (BOT), NMB, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ),SACCOS na vyama vya ushirika.