NA MWANDISHI WETU

WAKATI waislamu wa Zanzibar wakitarajiwa kuungana na wenzao duniani kote kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, serikali imewaonya wafanyabiashara watakaopandisha bei za vyakula hususani vinavyotumika kwenye mfungo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Darajani,Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema watakaopandisha bei hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

 “Mimi binafsi nitazunguka katika maeneo mbalimbali ya biashara kujiridhisha kama kweli wafanyabishara wanafuata maeekezo ya serikali na ijulikane kwamba zipo adhabu kali kwa watakaokiuka taratibu,” alisema.

Ili kuhakikisha bei hazipandi, Waziri Shaaban alisema wameunda kikosi kazi kinachoshirikisha Tume ya ushindani kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo na kuchukua hatua zinazostahili.

Licha ya sheria ya ushindani na kumlinda mlaji namba tano ya mwaka 2018 kutobainisha adhabu anazotakiwa kuchukuliwa anaekwenda kinyume, Waziri huyo alisema faini watakayotozwa inaweza isiwe chini ya shilingi milioni moja.

“Kumekuwepo na tabia ya muda mrefu ya baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa kutumia fursa ya mwezi mtukufu kupandisha bei kiholela hasa kwa bidhaa muhimu kama mchele, sukari na ngano.    Tabia kama hizi kutaka kuchuma faida kupitia mgongo wa wanaofunga hazikubaliki na mara nyingi husababisha wananchi wenye wa maisha duni kutekeleza ibada yao ya funga katika mazingira magumu,” alisema

Kuhusu kupunguza kodi za bidhaa kama ambavyo huwa inafanyika kila mwezi mtukufu, Shaabani alisema safari hii hawajaondoa kodi kwa sababu inaonekana hata serikali inapoondoa kodi hizo wafanyabiashara huwa hawashushi bei.

Katika mkutano huo Waziri huyo alitangaza bei elekezi ya bidhaa za mchele, ngano na sukari.

Alisema mchele wa mapembe utauzwa kwa shilingi 1,600 kwa kilo, sukari shilingi 2,000 kwa kilo na unga wa ngano utauzwa shilingi 1,600 kwa kilo.

“Bei hizi zitabaki hivyo kwenye masoko mpaka hapo zitakapofanyiwa mapitio na kutangazwa vyenginevyo na serikali,” alisema.

Naye mfanyabiashara maarufu visiwani humo Mohamed Raza, alisema wanaopandisha bei za vyakula hawana huruma na wananchi akidai bei

za vyakula na kodi bado hazijapanda.

 “Lazima tuwarahisishie wananchi kujikimu, waweze kula futari sio sisi (wafanyabiashara) kutumia fursa hii kuwakomoa, ushuru bao upo vilevile bei sokoni inakubalika ipo vilevile, tuwasaidie wananchi wapo wanaokula mlo mmoja kwa sababu hawana uwezo,” alisema.