LONDON, England

KOCHA Mkuu wa Tottenham, Jose Mourinho amezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumapili baada ya kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer, kutoa maoni binafsi dhidi ya kitendo cha Son Heung-min kilichopelekea kukataliwa kwa bao la Edinson Cavani.

Ole Gunnar hakufurahia kitendo cha nyota huyo wa Spurs, Son na baada ya mechi alimfuata na kumuambia ”Kama mtoto wangu angekaa chini kwa dakika tatu akihitaji wenzake 10 waje kumsaidia kuinuka, basi asingepata chakula.”

Kauli hiyo aliitoa baada ya Son Heung-min kukaa chini kwa dakika kadhaa kufuatia kuchezewa rafu na Scott McTominay mpaka Cavani anafunga bao akiwa hajainuka na ndipo bao hilo kukataliwa baada ya mwamuzi kupata msaada wa VAR.

Jose Mourinho ameonyesha kukerwa na maneno hayo ya Ole Gunnar na yeye kuamua kumjibu kwa kauli iliyozua gumzo kwenye mitandao ya kijamii ”Kwanza kabla ya yote wacha niwaambie kitu, nimeshangazwa na maoni ya Ole kwa Sonn na hamjaniuliza kuhusiana na hilo.”

”Nimemwambia Ole kuhusu hili tayari, kama ingekuwa mimi kumuambia mchezaji wa klabu nyingine A, B au C, kama angekuwa mtoto wangu nisingempa chakula cha usiku, unadhani ni kauli ya namna gani ?.”

”Nataka kusema kwa Sonn, ana bahati sana kuwa na baba bora kuliko Ole. Mimi ni baba, nafikiri kama baba siku zote utahakikisha una chakula cha kumpatia mtoto wako, bila kujali kitu gani anafanya. Hata kama ni kuiba basi utakuwa tayari kuiba lakini mtoto wako ale.”

Katika mchezo huo Manchester United ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3 – 1 dhidi ya Tottenham.