JUBA, SUDAN KUSINI
TAARIFA kutoka nchini Sudan Kusini zinaeleza kuwa wizara ya afya nchini humo imelazimika kutupa chanjo ya ugonjwa wa corona ambayo imebainika kupitwa na muda wa matumizi.
Msimamizi wa chanjo ya ugonjwa wa corona katika wizara ya afya ya Sudan Kusini, alisema walipopokea chanjo hizo waligundua baadae kwamba ni lazima zitumiwe katika muda wa siku 14 vinginevyo zitakua zimepitwa na muda.
Maofisa wa wizara ya afya nchini Sudan Kusini walisema wanalazimika kuzitupa dozi 60,000 za chanjo ya kupambana na ugonjwa wa covid-19 zilizotengenezwa na kampuni ya Oxford na AstraZeneca.
Alisema mbali ya kupitwa na muda chanjo hiyo ya AstraZeneca iliwatia wasiwasi wananchi wa taifa hilo kufuatia matatizo yanayotokana na dawa hiyo hasa baada ya kuwepo ripoti kwamba inasababisha kuganda kwa damu.
Chanjo hiyo ya AstraZeneca ilitolewa kama msaada na kampuni ya mawasliano ya MTN na Umoja wa Afrika mnamo mwezi Machi mwaka huu.
Richard Lako msimamizi wa Covid-19 katika wizara ya afya ya Sudan Kusini alisema walipopokea chanjo hizo waligundua baadae kwamba ni lazima zitumiwe katika muda wa siku 14 vinginevyo zitakua zimepitwa na muda.
Lako alisema kuwa hawana jinsi ni kwamba lazima chanjo hiyo itupwe na haipaswi kutumika kwani inaweza kusababisha maradhara zaidi.
Sudan Kusini ilipokea dozi zingine 432,000 za dawa hiyo mwishoni mwa mwezi Machi chini ya mpango wa kimataifa wa COVAX, lakini mpango wa kuwapa watu chanjo ulicheleweshwa na hadi wakati huu anasema ni watu 2,000 pekee ndio waliopatiwa chanjo.