UONGOZI bora na ushirikiano kati ya viongozi na watendaji wa chini katika taasisi yoyote, ndiyo njia nzuri ya kuleta ufanisi katika shughuli za taasisi hiyo.
Daima, kiongozi wa taasisi, iwe ya umma au binafsi, kampuni au idara, anapaswa awe mfano wa kuigwa na wafanyakazi walio chini yake.
Kutarajia kupata ufanisi katika kazi bila kwanza kujenga mazingira ya kuwezesha kupatikana kwake, ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
Kiongozi anaekabidhiwa majukumu ya kusimamia taasisi yoyote ile, anatakiwa ajue kwamba misingi ya uongozi ni pamoja na kukubali ushauri, kukosolewa na kusikiliza wengine.
Kuna kitu kimoja mara nyingi viongozi wa taasisi huwa wanajisahau na kujisahau kwa kudhani kuwa wanajua sana kiasi kwamba wafanyakazi wa chini hawana walijualo.
Kiongozi aliyefikia hatua hii, basi ameingia kwenye wale wenye mawazo mgando, kwani inawezekana kabisa mtu asiwe na stashahada wala shahada, lakini ana mawazo mazuri ya kimaendeleo.
Tumeiona mifano kadhaa watu waliofika darasa la nane la mkoloni ambao hata geti la Chuo Kikuu hawajawahi kuliona wakiwaelekeza kazi wale wenye madigirii kutokana na kubobea kwenye uzoefu.
Huu ni mfano halisa unaothibitisha kwamba uzoefu kutoka kwa mtu makini una faida na unaweza kuwa msaada mkubwa wa kimaendeleo katika taasisi na idara zetu.
Hatusemi kwamba kiongozi ofisini analazimika kuyafuata mawazo ya kila mtu ofisini, lahasha! Kwa sababu wapo wengine wanamashahada yananing’inia, lakini hawana waliwezalo na hata mawazo wanayoyatoa halengi kujenga.
Aidha si vyema kiongozi kuukimbia ushahuri ambao una lengo la kujenga na kuleta maendeleo ya taasisi ‘constructive’, lakini kwa bahati mbaya sana wapo baadhi ya watendaji kwa sababu ya shahada zao huwepo ofisini kubomoa na kuharibu kila linalofanywa ‘destructive’.
Tungependa kuwaona viongozi wa taasisi zetu kwenye mashirika, idara na kwenye mamlaka za umma, wanakuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ni ubunifu tu utakaofanywa na taasisi katika utoaji wa huduma za umma ndio utakao wafanya wananchi waweze kuridhika na utendaji wa serikali yao.
Tunachotaka kueleza ambacho ni sahihi kabisa ni kwamba pale taasisi inaposhindwa kutekeleza majukumu yake bila ya sababu za msingi maana yake ni kwamba serikali imeshindwa kuwajibika katika eneo hilo.
Kiongozi mwenye busara hapendi kuona serikali inashindwa kwenye eneo lake, bali hukomaa kuongeza kasi jinsi anavyoweza kukabiliana na changamoto zilizopo.
Kabla ya taasisi kufikia hatua ya kushindwa kiongozi wa taasisi anatakiwa kukaa chini na watendaji wake kuangalia tatizo liko wapi, kama lipo ndani ya uwezo wao wakae walitatue.
Tunafahamu vyema zipo changamoto nyengine zinazoweza kutatuliwa na serikali kuu, hivyo kiongozi hupaswi kukaa nazo kwenye makaratasi ofisini, kwasababu hazitopata ufumbuzi.