TAKRIBANI watu 34 wamekufa maji baada ya boti kupinduka katika pwani ya nchini Djibouti, Shirika la Uhamiaji duniani (IOM) limeeleza.

Boti hiyo ”iliyokuwa ikiendeshwa na wasafirisha watu” ilikuwa imebeba wahamiaji takribani 60 waliokuwa wakikimbia mzozo wa Yemen na waliokuwa njiani kwenda Djibouti, kwa mujibu wa IOM.

Haifahamiki chanzo cha chombo hicho kupinduka, lilisema shirika hilo.

Shirika hilo limeeleza kuhusu hali ya maelfu ya wahamiaji wa Kiafrika wanaofanya safari za hatari kutoka pembe ya Afrika kwenda nchi za Ghuba wakitafuta ajira.

Limesema ugonjwa wa Covid-19 umesababisha watu wengi kurejea kwenye nchi zao kwasababu mipaka mingi imefungwa kutokana na janga hilo.

IOM imesema maelfu wamekwama nchini Yemen, wengi wakiishi kwenye ” mazingira ya hatari”- na wamekuwa wakilazimika kuwalipa wasafirishaji binadamu kurejea nyumbani.

Mwezi uliopita, takribani wahamiaji 20 walikufa baada ya wasafirishaji hao kuwasukuma watu 80 miongoni mwao pwani ya Djibouti.