NA JUMBE ISMAILLY, SINGIDA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, imempandisha kizimbani, Mchumi wa Mkoa wa Mbeya, Halima Ajali Mpita, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida.
Mchumi huyo alipandishwa Mahakamani kwa tuhuma za kuisababishia serikali hasara ya shilingi milioni 33,100,000/= kwa kufanya malipo ya mbao hewa kwenye shule za sekondari katika Wilaya ya Iramba.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda aliyasema hayo kwenye taarifa ya kuanzia mwezi Januari hadi Machi, mwaka huu, aliyotoa kwa waandishi wa habari.
Elinipenda wengine waliopandishwa kizimbani na Halima Ajali Mpita, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.
Wengine alisema ni pamoja na aliyekuwa Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Stephen Pundile, aliyekuwa Afisa Takwimu, Zakia Maulid Ituja, wakishirikiana na Mkurugenzi wa Kampuni binafsi ya Nicholaus Maro &General Suplies, Nicholaus Maro.
Mkuu huyo wa taasisi hiyo, aliweka wazi kwamba taasisi hiyo ni chombo chenye kusimamia mapambano dhidi ya rushwa nchini ikiongozwa na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Mkuu huyo wa TAKUKURU amebainisha kuwa taasisi hiyo iliwafikisha katika Mahakama ya wilaya ya Iramba, Simion Mkumbo Shango, na Joseph Kingu Shani, kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ya shilingi 1,025,000.
Fedha hizo, alisema zilitokana na kukubalina kulipana kiasi hicho cha fedha, ili wasiweze kumchukulia hatua mzazi wa binti ambaye mtoto wake alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi wa kidato cha nne.
Mkuu wa TAKUKURU huyo Mkoa wa Singida, katika kesi ya jinai namba 4 ya mwaka 2020 ilimhusu Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kinyarimi,wilayani Ikungi, John Ambrose Mbua aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kushawishi rushwa ya shilingi 150,000 na kupokea shilingi 100,000 ili amsaidie fundi aliyekuwa na madai aweze kulipwa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Elinipenda katika hukumu yake iliyotolewa na Mahakama hiyo, mshitakiwa huyo alihukumiwa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 500,000 au kwenda kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela.