NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

CHAMA Cha wafanyabiashara mkoa wa Arusha (TCCIA)   kimeanza kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara wa  nyama katika jiji la Arusha, namna ya kuendesha  biashara zao na kuondoa migongano iliyopo na mamlaka za Nyama nchini.

Akizungumza na vyombo vya habari Katika warsha hiyo,iliyofanyika jijini hapa, mwezeshaji wa TCCIA, Charles Makoi amesema kwamba TCCIA imelazimika kuwawezesha  wafanyabiasha hao kupata mafunzo yatakayowasaidia kutambua Sheria na taratibu za uuzaji wa Nyama na hivyo kuondoa malalamiko yanayojitokeza baina yao na Bodi ya Nyama.

Amesema TCCIA inatamani kuona wafanyabiashara wa nyama Mkoani hapa wanafanya kazi zao katika mazingira Safi na salama kwa kufuata sheria na kama kuna maeneo wanavuka mipaka basi bodi ya nyama iweze kuwapa maelezo na taratibu za kufuata kufanya kazi kwa urais.

“Mafunzo haya yanaendeshwa na maofisa wa bodi ya Nyama lengo ni kuona namna ya kuondoa Changamoto Kati ya wadau wa nyama na Bodi ya Nyama “alisema

Aidha ameitaka bodi ya Nyama nchini kusogeza huduma zake kwa kufungua ofisi katika mkoa wa Arusha, ili kuwezesha wafanyabiashara wa nyama kutambua mapema mabadiliko ya sheria za nyama.

“Tumepokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara wa Nyama na wakilalamikia mabadiliko mengi ya sheria ya Nyama hivyo  tumeona tuwakutanishe na bodi ya nyama waweze kujadili kwa pamoja na kuweka mikakati ya uendeshaji biashara alisema Makoi 

Awali akiendesha warsha hiyo Afisa Nyama kutoka bodi ya Nyama Tanzania, Edgar Mamboi, amesema miongoni mwa changamoto walizogundua kwa wadau wa Nyama ni ukosefu wa Elimu ya Nyama na Masoko pamoja na ukosefu wa mifugo Bora ya Nyama .

Amesema kuwa bodi ya Nyama imejipanga kuimarisha mifumo ya biashara ya Nyama nchini ,usajiri ,masoko na Mawasiliano ili kuwa karibu na wafanyabiashara wa Nyama ikiwemo kuwasogezea huduma kwa kufungua ofisi za kanda na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata Nyama.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa mifugo pamoja na bei ambazo zimekua sio rasmi hivyo kupeleka kuyumba kwa masoko ya nyama hivyo wao kama bodi wameyapokea na kwenda kufanya kazi mapema hili kunusuru sekta hiyo kupoteza mapato.