NA KHAMISUU ABDALLAH

ZANZIBAR ni nchi iliyojaaliwa na rasilimali nyingi ikiwemo rasimali ya bahari na hata ardhi yake kukubali kilimo.

Mara nyingi katika vizazi vya wakati huu wa sanyansi na teknolokujia wananchi wengi wa visiwa vya Unguja na Pemba wameondoka katika utamaduni wao hasa wa kula vyakula vya asili kama vile muhogo, viazi, ndizi na nafaka nyengine na kujikita katika kula vyakula vya makopo.

Takwimu zinaonesha kuwa maradhi yasioambukiza yanachukua nafasi ya kwanza kwa Zanzibar kupoteza vifo vya watu kutokana watu kutokubali kubadili tabia zao.     

Utafiti uliofanywa mwaka 2011 ulionesha kuwa Zanzibar ugonjwa wa shinikizo la damu upo kwa asilimia 33 na maradhi ya kisukari asimilia 3.7.

Aidha maradhi hayo yanatajwa kama ndio kisababishi cha maradhi mengine kama vile tenzi dume kwa wanaumme na saratani ya matiti kwa wanawake.

Zanzibar kama ilivyo sehemu kubwa ya dunia, saratani zinazoongoza ni saratani ya matiti kwa wanawake, saratani ya tezi dume na saratani ya shingo ya mlango wa kizazi.

Maradhi hayo kwa kiasi kikubwa hupelekea vifo na idadi kubwa ya watu wanaougua kutokana na watu wengi kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao na pale wanapokwenda hospitali wanakuwa wameshathirika.

Aidha ugonjwa wa kisukari unachukua nafasi ya kwanza kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa hao siku hadi siku inayosababishwa na jamii kutokubali kubadili mfumo wa maisha yao.

Aidha kwa upande wa mbogamboga na matunda imebainika kuwa asilimia 98 ya wananchi wa Zanzibar hawali mbogamboga na matunda hali ambayo inapelekea kuongezeka kwa maradhi hayo..

Aidha serikali na jumuiya mbalimbali zimekuwa zikielimisha jamiii juu ya umuhimu wa kupima afya mara kwa mara ili mwananchi aweze kufahamu mapema

Bado jamii kubwa ya Zanzibar ina usiri sana kwenda kupima afya zao hasa saratani kwa kuhofia kupata ulemavu ikiwemo wanawake kutolewa baadhi ya viungo vilivyoanza kuathirika.

Imefika wakati wananchi kuachana na dhana hiyo na kwenda vituo vya afya kuchunguza afya zao mapema kwani wanapojua hali za afya zao wanaweza kuishi kwa matumaini.

Kitendo cha kuchunguza afya mara kwa mara kinamuweka huru mtu wakati wote kuwa salama katika mwili wake kwani waswahili wanasema ‘kinga ni bora kuliko tiba’.

Hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kupima afya yake mara kwa mara ili aweze kujijua na pale anapogundulika aweze kupatiwa matibabu ya haraka.

Ili mtu awe na afya bora anatakiwa kutumia matunda kwani ndani yake kuna mchanganyiko wa vitu mbalimbali na kurejea katika kula vyakula vya asili waliokuwa wakila wazee wetu ili kuepusha maradhi yanayoweza kuepukika ikiwemo maradhi yasioambukiza.

Kila mwananchi ana wajibu wa kuunga mkono jitihada za serikali na taasisi zisizo za kiserikali katika kupunguza idadi ya wagonjwa wa maradhi yasioambukiza visiwani Zanzibar.