NA AMEIR KHALID

MBUNGE wa Jimbo la Chwaka, Haji Makame Mlenge, amesema ataendelea kuwa bega kwa bega na wana kikundi wa Hakiweki katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Mlenge alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanakikundi hao na kuwapa pole baada ya kuwatembelea na kuona uharibifu mkubwa wa mazao yao katika shamba lao uliotokana na uhaba wa maji.

Alisema ameumizwa na hali halisi iliyotokea ambapo siku za nyuma alipotembelea shamba hilo, alipewa changamoto ya uhaba wa maji, wakati akilitafutia ufumbuzi yakataokea yaliotokea.

‘’Leo nimekuja kuwapa pole na kusaidia kuondosha tatizo hili ili shamba lipate na maji na kuendelea kutafuta njia mbadala za kuondosha hilo’’alisema.

‘’Suala la umeme bado naendelea kulifanyia kazi licha ya kuwa hivi sasa haliwezi kutatuka kwa haraka, lakini jitihada zinaendelea ili kuhakikisha wanapata umeme kwa siku zijazo.

Ameliomba Shirika la Umeme Zanzibar ( ZECO) kujitahidi kupanga ratiba ambazo zinaweza kutekelezeka hasa katika kuwasaidia wananchi kwa kuhakikisha wanaondosha kasoro zilizopo ili kuwaondoshea shida ya umeme wananchi.

Hata hivyo, alisema atahakikisha anaendelea kusaidia pamoja na viukundi vyengine, ili kuhakikisha wanachama wake wanakomboka na umasikini kupitia kilimo chao cha tungule.

Aliwataka wanakindi hao kujitahidi na kuhakikisha wanakwenda na malengo ya baadaye ili kupata mafanikio zaidi.

Nao wanachama wa  ushirika huo walisema  uhaba wa maji umewaathiri sana licha ya kununua pampu ya kusukumia maji lakini hawakufikia malengo, kwa saabau ya ukubwa wa shamba na udogo wa pampu jambo ambalo liliwaathiri.

‘’Kilimo kilikuwa kizuri tunavuna tungule kwa wingi na kupata kipatao kikubwa sana lakini hivi sasa tumepata hasara kubwa kutokana na tatizo hilo ila hatujakata tamaa na tunaendelea na kilimo chetu’walisema.

Katibu Salum Muhsin Amour, alisema ushirika wao hawakuvuna kama kawaida yao Jambo ambalo limewapelekea kupata hasara isiyopungua shilingi milioni 10, ambapo kawaidia wanapovuna hupata zaidi ya milioni 18 na kuendelea.