Lengo ni kuleta maendeleo ya huduma za kijamii

NA BAKARI MUSSA, PEMBA

ZANZIBAR kama zilivyo nchi nyengine duniani nayo inategemea mambo mbalimbali katika kuendesha uchumi wake.

Sambamba na hilo lakini pia uchumi huo unaendanna na kuleta maendeleo tofauti yakiwemo ya huduma za kijamii kama vile huduma za maji safi na salama, afya, nishati, miundombinu ya barabara, elimu na mengi mengineyo.

Kwa miongo kadhaa Zanzibar ilitegemea mazao ya biashara kwa ajili ya kuendesha nchi ikiwa ni pamoja na nazi na karafuu.

 Lakini mnamo miaka ya 1990 mwanzo mazao hayo yaliporomoka bei katika masoko ya dunia jambo ambalo Zanzibar ilijipanga upya kutafuta njia gani ya kuongeza mapato yake hasa katika suala la kupata fedha za kigeni.

Kwa sasa miongoni mwa sekta iuliyopewa kipaumbele ni utalii ambao huchangia asilimia 27 ya pato la taifa ikifuatiwa na ukusanyaji wa kodi mbalimbali.

Hivyo chini ya Serikali ya awamu ya saba ya Dk. Hussein Ali Mwinyi imeimarisha sekta ya kodi ili kuona wafanyabiashara na taasisi nyengine zinalipa kodi kwa ajili ya kuleta maendeleo ya nchi.

Kodi ni moja ya nyenzo muhimu ambayo inaiwezesha Serikali kupanga mipango yake ya maendeleo hivyo lazima mkakati wa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali upewe kipao mbele na wale wenye jukumu hilo wawajibike ipasavyo.

Katika hotuba zake mbali mbali alizowahi kuzitowa kweny utawala wake, ikiwemo ile ya uzinduzi wa baraza la Wawakilishi, uteuzi wa mawaziri , makatibu wakuu na ile ya Mapinduzi hakusita kuliwekea mkazo suala hilo.

Lakini kama hiyo haitoshi katika hotuba zake za mwanzo wakati akisalimiana na wananchi waliomchaguwa alisisitiza suala hilo kwa kusema.-

 “WanaCCM naomba munivumilie kwa mutakayo yasikia nimekusudia kuchukuwa maamuzi magumu juu ya fedha za umma ili hapo baadae fedha za umma ziweze kuheshimiwa”, alisema.

Alifahamisha kuna fedha nyingi za miradi, ikiwemo za ZUSP, Maji na muendelezo wa ZUSP kama fedha hizo hatukuzifanyia hivyo basi zitaharibiwa kwa faida ya wachache.

Kama hiyo haitoshi Dk, Mwinyi amelivalia njuga suala la ukusanyaji wa mapato kwani alilowaahidi wananchi wa Zanzibar katika Kampeni zake kulitekeleza kwa haraka ni kukuza uchumi.

Alisema atasimamia kusimamia na kuongeza pato la Taifa kutoka thamani ya shilingi trilioni 2.4 mwaka 2015 hadi kufikia thamani ya shilingi trilioni 3.1 mwaka 2019.

Sambamba na hilo atasimamia  kuongezeka makusanyo ya ndani, kutoka shilingi bilioni 428.511 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 748.9 mwaka 2019 pamoja na kupunguza utegemezi wa bajeti na kufikia asilimia 5.7 na kuvuuka lengo linaloanishwa na kufikia asilimia 7.

Hata hivyo katika hotuba ya Dk. Mwinyi wakati akilizinduwa Baraza la kumi la Wawakilishi, katika suala zima la Kodi alisema, “ Ili tuweze kutekeleza kwa ufanisi ujenzi wa uchumi mpya ni lazima tuongeze uwezo wetu wa kukusanya Kodi”, nanukuu .

Alieleza Serikali ya awamu ya nane itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato,kwa kuhakikisha kwamba kila mtu anaestahili kulipa kodi analipakodi stahiki .

Aidha atahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutowa huduma bora zaidi kwa wananchi.

“Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi”hotuba hiyo ilieleza.

Hili lilionekana kama miujizi kwa wakati huo, na ndio maana wapo wananchi na hasa wafanyabiasha walioshindwa kuamini kuwa, kunaweza kuwa na punguzo la kodi.

“Nawaahidi leo kweupe mchana, kwamba nichaguweni niwe rais wa Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine nitahakikisha napunguza kodi na matozo mengine,” alisema wakati huo.

Dk, Mwinyi alifafanua kuwa, kuwepo kwa kodi kubwa umekuwa haushawishi wafanyabiashara kulipa kodi hizo kwa wakati.

Ndio maana alitamani kuwa, lazima kuwepo kwa kodi ndogo ambazo hizo zitakwendana na maisha ya wafanyabiashara na kuwahamasisha walio wengi kulipa kodi.

“Mimi ninachoaamini kuwa, tukiwa na kodi na matozo mengine hapo uchumi wetu unaweza kupanda kwa haraka, kwani hizo huwashawishi waliowengi kulipa,’’alisema.

Alisema anaamini uchumi wa Zanzibar unaweza kupaa na kubadili maisha ya watu wake, kwa kule kulipwa kodi ndogo ambazo ndio zilizoko katika nchi kadhaa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha AAFP Taifa, Said Soud Said alisema kauli za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi, kuhusiana na usimamizi wa Kodi ni suala muafaka kwani hakuna taifa lolote Duniani linalokwenda bila ya kutegemea Kodi.

Aliwataka Wananchi na walipa kodi kwa ujumla kumuunga mkono Rais kwa kuhakikisha kila mwenye haki ya kulipa kodi anafanya hivyo kwa ajili ya kuisaidia Serikali katika kupanga mipango yake ya maendeleo.

“Nampongeza Rais Dk, Mwinyi kupambana na watu wanaohujumu uchumi na kuwachukulia hatuwa wale wote kwa maana nyengine wanatuhumiwa kuhujumu uchumi kwani hizo ni pesa za kodi za wananchi”, alisema.

Alisema anaamini kauli za Dk, Mwinyi alizokuwa anazitowa katika mikutano ya Kampeni kuhusiana na kupunguza kodi imekidhi haja pale ZRB ilipoanza kuchukuwa hatuwa ya kupunguza kodi ya VAT kutoka 18% hadi 15%.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na mipango, Jamal Kassim Ali alisema, wakati akitoa hotuba fupi baada  ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo la ZSSF huko Tibirinzi, alisema hayo  ni mafanikio makubwa kwani kutaongeza ufanisi  wa utendaji  huduma   na kuongezeka kwa mapato.

Alisistiza kuwa wale wote watakaopangishwa katika jengo hilo wahakikishe wanalipa kodi ili fedha hizo ziweze kurudi na kuleta tija kwa wananchi.

Nae Meneja wa TRA Pemba, Habibu Saleh Sultan,akilizungumzia suala la usimamizi wa kodi Zanzibar aliiambia makala hii kwamba utawala wa Dk, Hussein Ali Mwinyi, kumekuwa na mafanikio makubwa ya ukusanyaji wa mapato kisiwani humo .

Alisema Wafanyabiashara wa Pemba wameweza kuruhusiwa kuingiza na kuteremsha mizigo moja kwa moja kutoka nje ya nchi na wameshaanza kufanya hivyo na hivyo kuongezeka kwa ulipaji wa Kodi.

Alifahamisha pamoja na hilo pia wafanyabiashara wamehamasika kulipia kodi kwa hiari baada ya kuona kodi wanazolipia zinawafaidisha kwa maendeleo mbali mbali ndani ya Kisiwa cha Pemba.

“Uchumi wa ndani umekuwa na kutokana na mizigo kutoka nje hata 40% kwa upande wa uthamini wa magari inawapa fursa waigizaji wa magari kuingiza Pemba moja kwa moja”, alisema.

Alieleza ili kuunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar Dk, Mwinyi, kusimamia ulipaji kodi, aliwataka wafanya biashara kutumia fursa zilizopo kuingiza mizigo moja kwa moja kutoka nje ya Pemba kisiwani humo ili kodi wanazolipa ziwafikie wananchi wa ndani ya nchi yao.

Aliishauri Serikali ili kodi ziongezeke kuna haja ya kutilia mkazo na udhibiti wa raslimali za Baharini kama vile Kamba, Pweza, ngisi, Mwani , Samaki, chumvi ili idara ya kodi za ndani iweze kukusanya kodi zitokanazo na raslimali hiyo na hata kilimo cha mpira ambacho kinaonekana kuzalishwa kwa wingi Pemba.

“Hizi ni biashara ambazo hazijapewa kipao mbele na hivyo kuna uwezekano usafirishaji wake hauko kisheria ingawaje unafanyika na hivyo sio rahisi sana kupatikana kodi zake”, alishauri.

Kwa upande wa Wananchi wamempongeza Dk, Hussein Mwinyi, kwa kulitilia mkazo suala zima ukusanyaji wa kodi kwani inawapa faraja kuona kuna kiongozi anataka kuliondowa suala la ulipaji wa kodi ambazo hazifiki kunako husika kwa ajili ya maendeleo ya watu wote na hivyo kujinufaisha watu binafsi.

Walisema wamaeamini kuwa iwapo kodi zilikuwa na usimamizi mkubwa kama zilivyosasa ni wazi Zanzibar ingefikia uchumi wa kati mwanzo kabla ya Tanzania bara.

Hata hivyo, Wananchi hao walieleza kuwa wanaomba Serikali iwe na usimamizi mkubwa wa Kodi na pale inapoona kuna miongoni mwa watu wanarejesha nyuma juhudi hizo basi wachukuliwe hatuwa kama ilivyoanza.